Wafanyabiashara Wazishukia TRA, TPA na Tanesco Mbele ya JPM

Wafanyabiashara Wazishukia TRA, TPA na Tanesco Mbele ya JPM
Wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda nchini wameitupia lawama Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) pamoja na Shirika la Umeme (Tanesco) kwa kuchangia kurudisha nyuma biashara, uzalishaji na uagizaji wa bidhaa nchini.

Wametoa kauli hiyo leo Machi 19, 2018 katika mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara unaofanyika Ikulu Dar es Salaam na kuongozwa na mwenyekiti wa baraza hilo, Rais John Magufuli.

TRA imelalamikiwa katika mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya ukadiriaji, bandari kwa kuwa na tozo kubwa huku Tanesco ikitajwa kuwa kikwazo katika uchumi wa viwanda.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori  Tanzania (Tatoa), Angelina Ngalula ameomba Serikali kuangalia upya uwezekano wa malori kutoa huduma katika usambazaji wa mizigo inayoingia bandarini kwa ajili ya soko la Tanzania.

Mmiliki wa kiwanda cha nyama, John Chogo amesema vifungashio wamekuwa wakinunua nje ya nchi hatua inayochangia kuongeza gharama ya bidhaa zao kabla ya kuingia sokoni, hivyo amependekeza  kodi zipunguzwe.

Mmiliki wa kiwanda cha kusindika na kuzalisha mafuta ya alizeti cha Mount Meru Millers kilichopo mjini Singida, Atul Mittal amesema kasi ya Rais katika kuelekea uchumi wa viwanda inaweza kukwamishwa na wasaidizi wake.

Soma: TPSF yataka kero bandarini Dar kushughulikiwa

Mmoja kati ya wazalishaji wa kampuni binafsi za kuzalisha nishati ya umeme kutoka mkoani Rukwa aliyefahamika kwa jina moja la Kasiano amesema uzalishaji wa umeme umekwama  kutokana na urasimu wa Tanesco.

Kasiano ambaye ana uwezo wa kuzalisha megawati 360 amesema majadiliano na Tanesco yamechukua muda mrefu, hivyo amemwomba mwenyekiti wa baraza hilo kuingilia kati.

Makamu Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte amesema sekta ya umeme inaweza kukwamisha juhudi za uchumi wa viwanda.

Amesema kiwango cha wastani wa kuhudumia umeme kwa kila mtanzania bado kipo chini sana na hakiwezi kufanikisha juhudi hizo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad