Wakili Aliyeidhinisha Kiapo cha Odinga Azuiliwa Uwanja wa Ndege Nairobi

Wakili Aliyeidhinisha Kiapo cha Odinga Azuiliwa Uwanja wa Ndege Nairobi
Wakili wa upinzani aliyeidhinisha kiapo cha Bw Raila Odinga alipokuwa anajiapisha kuwa 'Rais wa Wananchi' mwezi Januari bado amekwama katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi.

Bw Miguna Miguna alijaribu kurejea Kenya Jumatatu lakini akazuiwa kuingia baada yake kudaiwa kutowasilisha pasipoti ya Canada ambayo ilitumiwa kumsafirisha kwa nguvu hadi Canada.

Taarifa zinasema Bw Miguna, ambaye pasipoti yake ya Kenya ilitwaliwa na polisi kabla ya kuondolewa kwake Kenya mwezi jana, alikuwa ametakiwa kuwasilisha ombi la kupata visa ya kukaa Kenya kwa miezi sita kwa kutumia pasipoti hiyo yake ya Canada.

Alikataa jaribio hilo na badala yake kutoa kitambulisho chake cha taifa kuonesha kwamba yeye ni Mkenya na kutaka aruhusiwe kuingia.

Bw Miguna, aliyekuwa amewasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mwendo wa saa nane adhuhuri, alikesha kwenye uwanja huo.

Maafisa walijaribu kumsafirisha kutoka uwanja huo kwa kutumia ndege ya shirika la Emirates ambayo ilikuwa inaelekea Canada kupitia Dubai.

Wakili wa upinzani James Orengo, seneta ambaye majuzi alichaguliwa kuwa kiongozi wa upinzani Bunge la Seneti, ameambia Reuters kwamba maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia ndio waliojaribu kumlazimisha Bw Miguna kupanda ndege hiyo iliyokuwa inaondoka.

Video iliyopeperushwa moja kwa moja na runinga ya kibinafsi ya Citizen ilimuonesha Bw Miguna akiwa kwenye lango la ndege akiwaambia wahudumu: "Siendi popote, hamuwezi kuniondoa kutoka kwa nchi yangu kwa nguvu."

Bw Orengo ameambia Reuters kwamba maafisa hao wa polisi baadaye walimuondoa mwanasiasa huyo kutoka kwenye ndege hiyo na kumzuilia kwa muda katika afisi za uhamiaji katika uwanja huo wa JKIA.

Baadaye asubuhi, walimhamishia kituo cha polisi cha uwanja huo na kuendelea kumzuilia.

Odinga kufika uwanja wa ndege
Bw Odinga alikuwa amefika uwanjani humo Jumatatu usiku kujaribu kutatua mzozo huo.

Kwa mujibu wa Bw Orengo, Bw Odinga alikuwa ametoa wito kwa serikali kumrejeshea Miguna pasipoti yake ya Kenya.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Uhamiaji mapema Jumanne ilisema Bw Miguna alianza "kuzua fujo na kulalamika" uwanja wa ndege na kwamba alikuwa anataka kuruhusiwa kuingia Kenya bila kuidhinishwa na maafisa wa uhamiaji.

Wizara hiyo imesema inafanikisha utaratibu wa kumuwezesha Bw Miguna kuwasilisha tena ombi la kuwa raia wa Kenya.

Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Joseph Munywoki kwenye taarifa alisema: "Badala ya kuonesha hati za kusafiria alizotumia kwenda Canada, Miguna alianza kuzua fujo na kulalamika akisema kwamba yeye ni Mkenya na anafaa kuruhusiwa kuingia Kenya bila kupitia kwa meza ya idara ya uhamiaji kama inavyotakiwa kwa abiria wote wanaowasili bila kujali uraia wao."

"Hatujamzuia kuingia Kenya, tunamtaka tu afuate utaratibu kama watu wengine wote," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani

Idara ya uhamiaji ya Kenya imekariri kuwa Miguna alipoteza uraia wa Kenya mwaka 1988 alipopewa uraia wa Canada wakati alipokuwa ni kinyume cha sheria kuwa na uraia wa nchi mbili nchini Kenya.

Kuzuiliwa kwa Bw Miguna kumejadiliwa pakubwa kwenye mitandao ya kijamii Kenya, baadhi wakiunga mkono hatua hiyo lakini wengine wakiwashutumu maafisa wa uwanja wa ndege na serikali.

Bw Miguna alikamatwa na polisi kwa mchango wake katika kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa "rais wa wananchi", hafla iliyofanyika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi mnamo 30 Januari.

Bw Miguna, ambaye pia ni wakili, ndiye aliyetia saini hati ya kiapo ya Bw Odinga.

Serikali ilikuwa imeeleza hatua hiyo ya kiongozi huyo wa upinzani kuwa uhaini wa hali ya juu.

Bw Odinga anadai kwamba alimshinda Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 8 Agosti ambao matokeo yake yalifutiliwa mbali na Mahakama ya Juu kwa sababu ya kutokea kwa kasoro nyingi.

Mahakama iliamuru uchaguzi mpya ufanyike lakini Bw Odinga akasusia uchaguzi huo mnamo 26 Oktoba.
Polisi nchini Kenya wamejipata tena wakishutumiwa kwa kuwapiga na kuwajeruhi waandishi wa habari wakiwa kazini.

Polisi waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia waliwashambulia waandishi wa habari wa magazeti na televisheni na wapiga picha Jumatatu usiku walipokuwa wakifuatilia taarifa kuhusu kurejea Kenya kwa Bw Miguna.

Maafisa hao, ambao hawakufurahishwa na ufuatiliaji wa vyombo vya habari wa taarifa ya kurejea kwa mwanasiasa huyo waligeuza hasira zao kwa waandishi wa habari na kuwaumiza baadhi yao.

Mpigapicha wa televisheni ya NTV aliachwa akiwa na majeraha yaliyokuwa yanavuja damu huku kamera na vifaa vyake vya matangazo ya moja kwa moja vikiharibiwa na maafisa hao wa usalama.

Alikuwa akitangaza tukio hilo moja kwa moja alipovamiwa na polisi

Mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Citizen Steven Letoo pia alijeruhiwa na vifaa vyake vikachukuliwa.


Amevitolea wito vyombo vya habari kuchukua hatua za kisheria dhidi ya maafisa husika na makamanda wao.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad