Muda mfupi baada ya TFF kutoa taarifa hiyo, Wambura naye alikutana na waandishi wa habari na kuzungumza.
Alisema kamati hiyo ya maadili haina mamlaka ya kisheria.
“Kisheria makamu wa rais hawezi kupelekwa Kamati ya Maadili ambayo inaundwa na watu wachache na badala yake mkutano mkuu ambao una wajumbe wengi walionichagua kuingia madarakani ndiyo wanapaswa kunihukumu.
“Kama hiyo kampuni iliyotajwa kwamba nimeghushi barua za malipo si inayo meneja wake, basi aje atoe ushahidi wa hicho kinachosemwa kwa sababu wakati kamati inakutana kujadili hakukuwa na shahidi yeyote zaidi ya wakili wangu, Emmanuel Muga.
“Sababu ya yote haya ni nafasi yangu ya makamu wa rais, pili ni ajira zilizopo ndani ya shirikisho, tatu ni kutokana na fedha za shirikisho kwani mimi ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya TFF.
“Niliwahi kumuambia rais (Wallace Karia) kwamba nafasi ya katibu mkuu inapaswa itangazwe wazi ili mwenye vigezo aweze kuajiriwa, hiyo ni kwa mujibu wa Katiba ya TFF, lakini sikujibiwa kitu.
“Katiba inaelekeza kwamba, anayepaswa kuwa katibu mkuu wa shirikisho hawezi kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
“Anayekaimu kwa sasa (Wilfred Kidao) yeye ni Mwenyekiti wa Chama cha Makocha Tanzania ambaye ni mjumbe wa mkutano mkuu, hivyo hana vigezo.
“Lakini pia kwenye masuala ya fedha ieleweke wazi kwamba kwa kuwa mimi ni mwenyekiti wa kamati ya fedha ndani ya shirikisho huwa naletewa jinsi fedha zinavyotumika na wanaoidhinisha ni wengine.
“Kwa kipindi ambacho tumeingia madarakani mpaka sasa, tumeweza kutumia zaidi ya Sh bilioni tatu ambazo hakuna cha maana sana kimefanyika.
“Utakuta wakati mwingine utaona Kombe la Shirikisho (FA) pamoja na Ligi ya Wanawake mechi zake zinaahirishwa kutokana na matatizo ya fedha.
“Niseme tu huu mkakati umepangwa kwa sababu mpaka Jumanne siku ambayo nasafiri sikupewa taarifa zozote za kutakiwa kwenye kikao hicho.
“Labda wanataka wanitoe ndiyo wapate nafuu ya kuzitumia hizo pesa. Mpaka sasa (jana mchana) sijapokea taarifa zozote juu ya kilichoamuliwa na kamati hiyo, nikishapata, nitaongea na vyombo vya habari.”
Awali kabla ya Wambura hajazungumza hayo, wakili wake ambaye ndiye aliyekuwa kwenye kikao hicho siku ya kwanza, alisema: “Barua ya wito haikupelekwa kwa muhusika kisheria kwani ilitakiwa apelekewe ofisini anapofanyia kazi, badala yake amepelekewa nyumbani kwake usiku siku moja kabla ya kikao kufanyika.
Makosa anayoshtakiwa Wambura ni
1.Kupokea/Kuchukuwa fedha za Shirikisho (TFF) za malipo ambayo hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha kanui za Maadili za TFF Toleo la 2013
2.Kughushi barua ya kueleza alipwe malipo ya Kampuni ya JEKC SYSTEM LIMITED huku akijua malipo hayo sio halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013
3.Kufanya Vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na Ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (Kama ilivyorekebishwa 2015)