Kundi la kigaidi la Boko Haram limeendelea kumshikilia msichana mmoja kati ya wasichana 111 waliotekwa katika shule ya bweni eneo la Dapchi nchini Nigeria.
Mkuu wa jeshi la polisi nchini humo amesema kuwa wanaendelea kufanya mazungumzo na kundi hilo na kwamba limeahidi kumuachia msichana huyo hivi karibuni.
Leah Sharibu, msichana mwenye umri wa miaka 15 hakuwa miongoni mwa wasichana 105 walioachiwa na kundi hilo Jumatano.
Imeelezwa kuwa msichana huyo aliendelea kushikiliwa kwa sababu alikataa kubadili dini yake kuwa muislam, kwa mujibu wa mama yake.
Aidha, wasichana wengine watano waliotekwa na kundi hilo wanaaminika kuwa walifariki walipojaribu kutoroka mikononi mwa magaidi hao.
Mkuu wa jeshi la polisi, Jenerali Muhammed Abubakar amesema kuwa ameahirisha ziara yake katika eneo la Dapchi ili asiingilie mpango wa makubaliano ya kuachiwa kwa msichana huyo.