Watuhumiwa Saba wa Wizi wa Korosho Wapandishwa Kizimbani

Watuhumiwa Saba wa  Wizi wa Korosho Wapandishwa Kizimbani
WATUHUMIWA saba raia  wa Zambia, leo Machi 7,  wamepandishwa katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na tuhuma za kula njama, wizi na utakatishaji wa fedha.


Wakisomewa  mashtaka  mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono, akisaidiana na wakili wa serikali mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi  watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Kirby Ng’andu, ambaye ni meneja uendeshaji wa kampuni ya Zambia Cargo and Logistics; Robert Christopher, wakala wa usafirishaji na Isihaka Ngubi, dereva;   Cathbert Mlugu, mlinzi;  Mrisho Mindu, Karani;  Giften John na Maulid Said.


Wamesomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi,  ambapo imedaiwa kuwa  kati ya Januari 26 na Februari 2 mwaka huu,  katika kampuni ya Zambia Cargo and Logistics iliyopo Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa la wizi.

Imedaiwa kuwa siku na mahali hapo, washtakiwa hao  waliiba katoni 700 za korosho zilizobanguliwa  zenye thamani ya Dola za Marekani 54,180 ambazo ni sawa na Sh. bn. 120.5 mali ya Barabara Trading Tanzania Ltd.



Imeelezwa kwamba  watuhumiwa hao wote pia walijihusisha na muamala unaohusiana na katoni hizo 700 za korosho zenye thamani hiyo ya fedha huku wakijua kuwa, mali hiyo ni zao lililotokana na kosa la wizi.



Watuhumiwa   wamekana kutenda makosa hayo na wamerudishwa rumande kwa kuwa shtaka la utakatishaji wa fedha halina dhamana na  wakili Kishenyi ameiambia mahakama kuwa upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi  imeahirishwa hadi , Machi 9 mwaka huu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad