Meneja wa WCB, Sallam SK amesema kabla ya kutoa ngoma zao huwa zinakaguliwa na mlezi wao ambao ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda.
Ameendelea kwa kusema bado hawaelewi sababu ya kufungiwa kwa ngoma hizo, hivyo mlevi wao ataweza kuliongelea hilo zaidi. Kupitia ukurasa wake wa Instagram Sallam SK ameandika;
Tumepigiwa simu na vyombo vya habari kila sehemu kuulizwa juu ya nyimbo mbili za Diamond kufungiwa, nimeona tukiwa kama taasisi huwaga tunafanya vitu kwa kutokukurupuka sie kamaWCB Wasafi tulipoona taasisi yetu inakuwa kubwa tukaomba ulezi kwa Mhe. Paul Makonda ambae ni kiongozi wa serikali mwenye kupenda maendeleo ya vijana.
Kwa hiyo nyimbo zote za WCB kabla ya kutoka lazima mlezi wetu azipitie, kuna nyimbo nyingi ameshazizuia na zinazotoka basi ameridhia yeye binafsi zitoke, kwahiyo sioni sababu ya nyimbo ya Hallelujah na Waka kufungiwa kama inavyosemekana maana sisi hatujapata barua ya kuwa nyimbo hizo zimefungiwa na kwa sababu ipi.
Kama kweli zimefungiwa basi mlezi wetu ataweza kuongea mengi zaidi yangu mimi.
Wiki iliyopita Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) ilitangaza kufungia baadhi ya nyimbo zilizooneka kutokuwa na maadili, miongoni mwa ngoma hizo ni Hallelujah ambayo Diamond ameshirikiana na Morgan Heritage na ile ya Waka aliyoshirikiana na Rick Ross.