Chama cha ACT Wazalendo leo Aprili 19, 2018 kimemjibu Katibu wa Itifaki na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuhusu sakata la upotevu wa trilioni 1.5 kama ilivyoeleza ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kutolea ufafanuzi juu ya pesa hizo.
Akiongea na Waandishi wa Habari katika ofisi za chama hicho Kijitonyama, jijini Dar es salaam, Ado Shaibu amesema kuwa Polepole amejikuta akizungumza masuala ya muhimu kwa kuingiza propaganda ili ACT Wazalendo waanze kujibizana naye lakini hilo hawatafanya wataendelea kuhoji hela zilikopotea.
Hata hivyo, Ndg. Shaibu amesema ACT Wazalendo wamekuja na hoja tano jinsi ya kuwadhibiti CCM ambao kwa maelezo yao wanataka kuzima sakata upotevu wa trilioni 1.5 kwa kuleta hoja nyepesi nyepesi za upotoshaji.
Juzi jumapili, Aprili 15, 2018, sisi ACT Wazalendo tulifanya uchambuzi wa
awali wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
ya ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za umma kwa mwaka
2016/17. Tunafurahi kuwa uchambuzi wetu juu ya masuala 8 ya hatari
kwenye taarifa ya CAG umepokelewa vyema, na umekuwa ni mjadala wa
kitaifa.
Katika masuala hayo 8 ya hatari tuliyoyaibua, suala la shilingi 1.5 trilioni
kutokujulikana zimetumikaje ndilo ambalo limegusa hisia za watanzania.
Kwa ujumla sehemu kubwa ya ufafanuzi wetu utajikita kwenye hoja hii, kwa
sababu ndiyo hoja iliyogusa zaidi hisia za watu, hivyo hata upotoshaji na
uzushi umefanyika zaidi kwenye hoja hii.
Aprili 15, ACT Wazalendo tulisema yafuatayo kuhusu jambo hili:
“6% ya Fedha zilizokusanywa na Serikali hazijulikani zilizokokwenda. Katika
ukaguzi wa Bajeti ya mwaka 2016/17, ambayo ni Bajeti ya kwanza ya
Serikali ya awamu ya tano, CAG ameonyesha kuwa kati ya Bajeti ya shilingi
29.5 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza kukusanya shilingi
25.3 trilioni tu kutoka vyanzo vyote vya kodi, vyanzo visivyo vya kodi,
mikopo ya ndani na nje, na misaada ya wahisani na washirika wa
maendeleo. Serikali ilishindwa kukusanya kiasi cha shilingi 4.2 trilioni, sawa
na 15% ya Bajeti yote ya mwaka 2016/17. Jambo la kushtusha na
linalohitaji majibu ya Serikali ni kwamba, CAG amegundua kuwa katika
fedha zote zilizokusanywa, shilingi 25.3 trilioni, ni shilingi 23.8 trilioni tu ndio
zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengine, matumizi
ya maendeleo na kulipa madeni yatokanayo na amana za serikali na riba.
Shilingi 1.5 trilioni zilizobaki hazijulikani zimekwenda wapi. Fedha hii
ambayo matumizi yake hayajulikani ni sawa na 6% ya Fedha zote
zilizokusanywa mwaka huo. Matrilioni haya ambayo Serikali imeyapoteza ni
zaidi ya mara mbili ya Bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka husika (672
bilioni)”.
Jana, Katibu Mwenezi wa CCM alizungumza nanyi wanahabari, ambapo
ukiacha matusi, kejeli, vitisho na kashfa, sehemu kubwa ya mkutano wake
ulijikita kwenye hoja hii. Maelezo yake ni kuwa shilingi 25.3 trilioni ni mapato
ghafi ya Serikali, yakiwa na fedha za Zanzibar shilingi 203.92 bilioni, pamoja
na Hela Tarajiwa (Receivables) shilingi 687.3 bilioni. Na hivyo basi, mapato
2
halisi ya Serikali yalikuwa ni shilingi 24.4 trilioni. Zaidi akifafanua kuwa CAG
alikuta matumizi ya shilingi 23.79 kwa sababu Serikali haikuwa imepokea
fedha zake za hati fungani iliyoiva, kiasi cha shilingi 697.85 bilioni.
Mahesabu haya yaliyotolewa na msemaji wa CCM ndio msimamo rasmi wa
chama hicho, na hivyo ndio msimamo rasmi wa Serikali ya chama hicho. Na
hivyo basi ni dhahiri kuwa chama hicho kinaikataa taarifa ya CAG,
kimeamua kufanya upotoshaji mkubwa, na kuwahadaa watanzania juu ya
ziliko shilingi 1.5 trilioni zao.
Hoja 6 za Ufafanuzi juu ya Upotoshaji wa CCM:
1. Chama Kidogo kama ACT Wazalendo Kinaweza Kufanya
Uchambuzi wa Ripoti ya CAG?
Mwenezi wa CCM ameeleza kuwa ACT Wazalendo ni chama kidogo,
chenye mbunge mmoja, hivyo hakina uwezo wa kufanya uchambuzi wa
ripoti ya CAG. Hoja hii ni dhaifu, na ni dhihaka ya kututoa kwenye mstari,
maana pia haelezi kuwa ili chama cha siasa kichambue ripoti ya CAG
kinapaswa kiwe na ukubwa kiasi gani na kiwe na wabunge wangapi, na
hasemi kwamba masharti hayo anayoyaweka ni kwa mujibu wa sheria gani
ya nchi!
Uchambuzi wa ripoti za CAG ni suala la kitaalam zaidi, hauna mahusino
kabisa na udogo au ukubwa wa chama cha siasa, au hata idadi ya wabunge
wake. Ili mtu, au kikundi cha watu (Chama cha Siasa) afanye/kifanye
uchambuzi wa ripoti ya CAG, yanahitajika mambo matatu muhimu, mosi ni
Weledi (Proffesionalism), pili ni Ujuzi (Skills), na tatu ni Uzoefu
(Experience). Hivyo uchambuzi wa ripoti hii si zao la ukubwa wa chama
wala idadi ya wabunge.
ACT Wazalendo tumekuwa chama pekee nchini, chenye utamaduni wa
kuchambua Bajeti Kuu ya Taifa pamoja na kutoa mapendekezo ya
maboresho yake. Tumefanya uchambuzi wa bajeti kuu zote mbili za Serikali
ya awamu ya 5, kiasi cha Serikali (kwa khofu) tu mwaka jana kuvamia na
kupiga marufuku mkutano wetu wa uchambuzi wa Bajeti. Hivyo ni dhahiri
kuwa tunao uwezo wa kuchambua ripoti hii ya CAG, kiasi cha kukhofiwa na
Serikali. Na sasa kukhofiwa na chama kinachoongoza Serikali (kikiomba
Polisi waje kutukamata).
Kiongozi wa Chama chetu, ndugu Zitto, ambaye aliongoza timu iliyofanya
uchambuzi wetu juu ya ripoti ya CAG, ni Mchumi Mweledi kitaaluma, ana
Ujuzi wa kutosha juu ya masuala ya Uchumi na Ukaguzi kutoka kwenye
vyuo mbalimbali nchini na vya nje ya nchi, na ana uzoefu wa miaka 8 wa
kuchambua taarifa za CAG kwa kuwa ameongoza Kamati za Bunge za
usimamizi wa hesabu za Serikali za POAC na PAC kwa miaka hiyo 8. Sifa
zote hizo zinatupa hadhi na heshima stahiki sisi ACT Wazalendo, pamoja
na kuwa chama kidogo tu chenye mbunge mmoja, kufanya uchambuzi wa
ripoti ya CAG.
3
2. Ukaguzi wa CAG ulihusu fedha ZILIZOKUSANYWA. Si Mapato
Ghafi wala Fedha Tarajiwa (Receivables).
Katika Kitabu cha Hesabu za Serikali Kuu, CAG ameonyesha kuwa
amekagua fedha za Makusanyo ZILIZOKUSANYWA na Serikali, na sio
Fedha zilizotarajiwa kukusanywa na Serikali, au Mapato GHAFI kama
alivyodai mwenezi wa CCM. CAG ameonyesha kuwa kwa mwaka 2016/17
Serikali ilipanga kukusanya shilingi 29.5 trilioni kutoka kwenye vyanzo vya
mapato yote; ya kodi, yasiyo ya kodi, mikopo ya ndani, pamoja na mikopo
ya nje na misaada ya wahisani (Ukurasa Na. 29 – Jedwali Na. 12:
Mchanganuo wa Bajeti ya Makusanyo).
CAG ameonyesha kuwa Serikali ilikusanya shilingi 25.3 trilioni, na
kushindwa kukusanya shilingi 4.2 trilioni, sawa na 14.33% ya Bajeti yote ya
mwaka 2016/17. (Uk. wa 30 na 31: Muhtasari wa Ukusanyaji wa Mapato ya
Fedha Zilizotolewa). Fedha hizi zilizokusanywa (shilingi 25.3 trilioni), CAG
aliziona, kwa kuwa ziliingia kwenye Hesabu Jumuifu za Taifa (Consolidated
Accounts).
CAG ameonyesha kuwa Serikali iliweza kukusanya shilingi 25.3 trilioni
kutoka vyanzo na mchanganuo ufuatao; vyanzo vya kodi (14.27 trilioni)
vyanzo visivyo vya kodi (2.072 trilioni), mikopo ya ndani (5.916 trilioni) na
mikopo nje, na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo (3.047
trilioni). Hayo yapo Ukurasa wa 32 (Kielelezo Na. 6: Mwenendo wa Mapato
ya Serikali kwa miaka minne).
Kwa ushahidi huo, utaona kuwa hakuna Fedha Ghafi kama ilivyo
propaganda ya mwenezi wa CCM, bali CAG alikagua fedha ambazo Serikali
imeshazikusanya. Na Serikali yenyewe imetoa ushahidi wa nyaraka juu ya
namna ilivyozikusanya fedha hizo, na CAG ameziona katika hesabu
jumuifu. Hivyo basi, katika shilingi 25.3 trilioni zilizokusanywa hakuna fedha
tarajiwa (receivables), na pia hakuna fedha ghafi.
3. Hakuna Fedha za Serikali ya Zanzibar, Zingekuwepo
Zingeripotiwa.
Mwaka wa fedha wa 2016/17 ulianza Julai 1, 2016 na kuisha Juni 30, 2017.
CAG hutoa muda wa miezi mitatu kwa taasisi zinazokaguliwa, ili ziweze
kurekebisha vitabu vyake vya hesabu na kuviandaa vyema kabla hajaanza
kuvikagua. Serikali Kuu iliwasilisha hesabu zake kwa CAG mwishoni mwa
Septemba, 2017, miezi mitatu tangu mwaka wa fedha wa 2016/17 uishe,
ikionyesha namna ilivyokusanya fedha, kiasi cha fedha zilichokusanywa,
kiasi cha fedha zilizotumika, na namna fedha hizo zilivyotumika.
CAG alifanya ukaguzi wake kuanzia mwezi Oktoba, 2017, na alifanya kikao
na taasisi alizozikagua (exit meeting), ili kufafanua hoja zilizoibuliwa kwenye
ukaguzi husika, Januari, 2018. Katika nyakati zote hizo, Serikali Kuu, kwa
barua na kwa nyaraka, haikuonyesha kuwa kuna fedha zozote za Zanzibar
ambazo imezikusanya na hivyo hazipaswi kuwemo katika makusanyo ya
shilingi 25.3 trilioni.
Kama kuna fedha za Zanzibar, Serikali ilikuwa na miezi mitatu ya
kuzionyesha (Julai – Septemba, 2017), na pia ilipata wasaa wa kukutana na
4
CAG kwenye kikao cha kujadili hoja alizoziibua (Exit Meeting), mwezi
Januari, 2018. Nyakati zote hizo, Serikali imeonyesha namna imezikusanya
shilingi 25.3 trilioni, kwa uwazi, na hakuna mahali imesema kuwa kuna
fedha za Zanzibar. Mwenezi wa CCM anapingana na Serikali yake?!
4. Hati Fungani za Serikali zimekaguliwa na CAG
CAG ameeleza yafuatayo katika ripoti yake; “Kati ya shilingi 23.5 trilioni
zilizokusanywa, shilingi 23.79 trilioni ndizo zilizotolewa kwaajili ya
mishahara ya watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na
fedha kwa ajili ya kulipa madeni yatokanayo na amana za Serikali pamoja
na riba”. (Uk. wa 34: Uchanganuzi wa Makadirio ya Mapato ya Kugharamia
Matumizi).
Kwa mujibu wa CAG, Serikali imeonyesha nyaraka za hati fungani zote
ilizouza (katika eneo la mikopo ya ndani, ambapo Serikali ilikopa bilioni 500
zaidi ya fedha ilizoomba kukopa na kuidhinishiwa na Bunge), shilingi 5.9
trilioni (ikiwa imeomba ruhusa ya kukopa shilingi 5.4 trilioni), na pia Serikali
ameonyesha kiasi cha madeni ya amana na riba ambacho imelipia kwenye
hati fungani hizo (Uk. 34 Ripoti ya CAG juu ya Serikali Kuu).
Labda tu mwenezi wa CCM haelewi ‘Hati Fungani’ ni nini. Ndio maana
anaropoka tu kuwa Serikali inasubiri hati fungani zake ziive ili iweze kulipwa
shilingi 697.85 bilioni zake. Kwanza Serikali ndio huuza hati fungani, watu,
makampuni, mabenki, taasisi na asasi ndio hununua hati fungani, na
zinapoiva hizo hati fungani, Serikali ndio hulipa amana na riba za iliowauzia
hati fungani. Sasa mwenezi wa CCM hajui hata jambo hili rahisi kuhusu
masuala ya kibenki?
Serikali hupata sehemu kubwa ya mikopo ya ndani kwa utaratibu wa kuuza
hati fungani, na hulipia hati fungani hizo (zilizoiva) kwa utaratibu wa kulipa
amana na riba. CAG ameonyesha namna mikopo ya ndani ilivyopatikana
kupitia hati fungani, na pia amefafanua namna madeni ya riba na amana za
hati fungani zilizoiva yalivyolipwa.
5. CCM na Serikali yake Hawaaminiki
Kutokana na ufafanuzi huo tulioutoa, mtaona kuwa CCM, kama ilivyo kwa
CAG, nao wanakiri kuwa Serikali ilikusanya shilingi 25.3 trilioni, na ikatumia
shilingi 23.8 trilioni, na kuonyesha kuwa, kama ilivyo kwa CAG, nao wanakiri
pia kuwa shilingi 1.5 trilioni hazionekani ziliko. Wao wamekwenda mbele
zaidi tu kwa kuamua kufanya propaganda zenye lengo la kuuhadaa umma
kwa kutengeneza sababu na matumizi hewa juu ya fedha hizo (Fedha za
Zanzibar, Receivables na Hati Fungani). Wao na Serikali yao wametuhadaa
mno, hawapaswi kuaminiwa tena na Watanzania.
Uchambuzi wetu juu ya ripoti ya CAG uliibua masuala 48, tuliamua kwanza
kuyaainisha yale masuala 8 ya hatari tuliyoyasema Aprili 15, 2018 kwa
sababu ya unyeti wake dhidi ya haya masuala mengine 40 yaliyobakia.
Masuala hayo 48 yatokanayo na ripoti hii ya CAG ni taswira juu ya udhaifu
wa Serikali ya awamu ya 5 katika kuongoza nchi yetu.
CAG ametuonyesha mapungufu makubwa mno ya Serikali, ameonyesha
hadaa za hali ya juu za Serikali, kufikia kiasi cha cha kupika takwimu na
kutangaza mapato feki ya kodi yanayokusanywa na TRA ili ipate sifa tu
5
kuwa inakusanya mapato zaidi, wakati ni kinyume na ukweli. Zaidi ripoti ya
CAG imetuonyesha namna maamuzi ya kukurupuka ya Serikali yanavyolitia
hasara Taifa.
Nitatoa mfano mmoja kwenye eneo hili, kwa mwaka mmoja tu wa Serikali
ya awamu ya 5, hasara linayoipata Shirika la Umeme nchini, TANESCO
imepanda kwa zaidi ya mara 2, ukuaji wa deni kwa mwaka mmoja tu ni zaidi
ya 175%, kutoka hasara ya shilingi 124.46 bilioni, chini ya Serikali ya
awamu ya 4, mpaka hasara ya shilingi 346.40 bilioni za Serikali hii ya
awamu ya 5.
Mapendekezo ya ACT Wazalendo ni yapi?
-Tumemwandikia Barua Spika wa Bunge, Kuomba Uchunguzi Maalum wa
Jambo hili
Sasa ni dhahiri kuwa fedha za watanzania, shilingi 1.5 trilioni, hazijulikani
ziliko, CAG ameonyesha jambo hilo kupitia ripoti yake, CCM, chama
kinachoongoza Serikali, nacho kimeonyesha hilo kupitia taarifa yake, zaidi
kimeonyesha hakina uwezo tena wa kuisimamia Serikali yake, kimeamua
kushiriki hadaa ili fedha zenu Watanzania zipotee. Hivyo basi vyama vya
Upinzani tunao wajibu wa kuhakikisha watanzania wanajua fedha zao
zimekwenda wapi.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama chetu, ndugu Yeremia Kulwa Maganja,
amemuandikia barua Spika wa Bunge, ndugu Job Ndugai, kumuomba atoe
kibali kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, PAC, ili ikutane, na
imuagize CAG afanye ukaguzi maalum juu ya zilikopelekwa fedha hizi. Ni
matarajio yetu kuwa Spika atazingatia ombi letu kwake, kwa sababu ya
unyeti wake kwa nchi yetu.
Tunatoa wito kwa watanzania wote, watokanao na vyama vyote vya siasa,
tuungane pamoja kupaza sauti juu ya jambo hili. Fedha hizi, shilingi 1.5
trilioni ni nyingi mno, zingeweza kutumika kukopesha shilingi 100 milioni
kwa kila kijiji katika vijiji 15,000 nchi nzima, na kutatua tatizo la ajira na mitaji
kwa vijana na kinamama, zingeweza kujenga hospitali 10 zenye hadhi kama
ya Mlongazila, na kutatua changamoto za sekta ya afya nchini. Zingeweza
pia kuwasomesha bure chuo kikuu, vijana wote wa Kitanzania wanaoomba
mikopo kwa sasa, kwa muda wa miaka minne mfululizo. Ni fedha nyingi
mno, tuungane kuhakikisha tunajua ziliko.
Ahsanteni Sana.
Ado Shaibu
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma,
ACT Wazalendo,
Aprili 19, 2018.
Dar es Salaam.