Alikiba, AY na Daimond Waziunganisha Tanzania na Kenya, Rwanda Pamoja na Uganda
0
April 20, 2018
Siku moja baada ya msanii Ali Kiba kufunga ndoa na Amina Khalef, raia kutoka nchini Kenya, sasa atakuwa msanii wa tatu kuunganisha familia katika nchi zinaoziunganisha Afrika Mashariki.
Jumuiya ya Afrika Mashariki inaunganishwa na nchi sita ambazo ni Tanzania, Rwanda, Burundi, Sudani Kusini, Burundi na Kenya.
Awali aliyeanza kuunganisha undugu ni msanii Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz ambaye alikuwa na mahusiano na mwanama raia wa Uganda , Zarina Hassan ‘Zari’ na kufanikiwa kuzaa naye watoto wawili, Tiffah na Nillan.
Japokuwa kwa sasa Zari na Diamond hawapo pamoja, lakini kitendo cha kuzaa watoto kinawaunganisha kama familia.
Baadaye msanii wa siku nyingi wa Bongo Fleva, Ambwene Yessayah 'AY ' alifunga ndoa na mchumba wake wa siku nyingi, Remy ambaye ni raia wa nchini Rwanda.
Wawili hao waalianza kufunga ndoa ya kimila Feb 11 mwaka huu na kufanya sherehe nyingine nchini Tanzania, Februari 24 katika Hoteli ya Golden Tulip na kuhudhuriwa na mastaa mbalimbali akiwemo Lady Jaydee, Mwana FA, Salama Jabir, Profesa Jay (Joseph Haule-Mbunge wa Mikumi), Fid Q na wengineo wengi.
Kama vile haitoshi jana Kiba naye alifuata nyayo za Diamond na AY, baada ya kufunga ndoa na Amina Khalef mjini Mombasa kutokana na mwanamke huyo kuwa raia wa Kenya.
Shughuli za harusi zilianza majira ya asubuhi kwa Kiba kufungishwa ndoa msikitini majira ya asubuhi na jioni kufuatiwa na sherehe kubwa katika ukumbi wa Diamond Jubilee uliopo nchini humo.
Diamond ampongeza Kiba
Hata hivyo, jana katika ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram, Diamond alimpongeza Kiba kwa hatua yake hiyo kwa kuandika “Wadau nimeambiwa King Kiba kaoa leo...mfikishieni Salam zangu za ndoa njema, na maisha yenye furaha, amani na baraka tele.”
Hii ni mara ya pili kwa Diamond kutaka kuonyesha hadharani kwamba hana bifu na msanii huyo kama watu ambavyo wamekuwa wakiwachukulia, ambapo mara ya kwanza ikiwa ni muda mfupi tangu kituo chao cha TV cha Wasafi kuanza kurusha matangazo walicheza na nyimbo za Kiba jambo ambalo lilizua gumzo mitandaoni.
Tags