Aliyegundua Madini ya Tanzanite Amshukuru Rais Magufuli kwa Kutambua Mchango Wake na Kumpa Milioni 100

Mgunduzi wa madini ya Tanzanite, Jumanne Ngoma ametoa ya moyoni baada ya Rais John Magufuli kusema Serikali inautambua mchango wake na kumpa Sh 100 milioni.

Akizungumza leo Aprili 6, wakati wa uzinduzi wa ukuta kuzungumza mgodi wa Tanzanite, Magufuli amesema atampa barua Mzee Ngoma ya kutambua mchango wake katika ugunduzi wa madini hayo yanayopatikana Tanzania pekee.

Mzee Ngoma alimshukuru Rais Magufuli na kusema alibaini kuwa kiongozi huyo amechaguliwa na Mungu tangu wakati wa kampeni za urais mwaka 2015.

“Ninakushukuru sana Rais, kwa heshima hii na kunitambua mimi kama mgunduzi wa madini, ni heshima kubwa kwangu na niseme kuwa wewe umechaguliwa na Mungu,” amesema na kuongeza:

“Wananchi wa Mirerani huyu ni Rais wa wanyonge, mimi nisingejulikana leo hii, hii ni furaha kubwa.”

 Mtoto wa Mzee Ngoma, Asha Ngoma naye ametoa neno katika hafla hiyo na kumshukuru Rais kwa kuusoma na kuufanyia kazi ujumbe wake wa simu aliomtumia Rais leo asubuhi saa 12 kasoro.

“Nikushukuru sana kwa sababu sikutegemea kama utausoma na kuufanyia kazi ujumbe wangu wa simu niliokutumia leo asubuhi. Naomba uendelee kuuthamini mchango wa mzee Ngoma na kuhakikisha madini ya Tanzanite yanaendelea kuwa na thamani,” amesema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad