Baba wa Marehemu Chacha Heche Suguta Aliyeuawa na Polisi Afunguka

Baba mdogo wa marehemu Chacha Heche Suguta ambaye pia ni mdogo wa Mbunge John Heche, Bwana Issa Suguta, amevitaka vyombo vya dola kulinda wananchi wake kama inavyopaswa, na kama wameshindwa basi iwaache wananchi wajilinde wenyewe kwa namna wanayoijua.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika  kituo cha polisi mara baada ya wananchi kukizingira kufuatia tukio hilo, Mzee Suguta amesema kwamba kama serikali imeshindwa kuwalinda wananchi wake, basi iwape uhuru wa kujilinda wenyewe.

Mzee Suguta ameendelea kwa kuitaka serikali ya awamu ya tano kuwatetea wanyonge pale inapobidi, kama ambavyo inajitangaza kuwa ni serikali ya wanyonge.

“Tunaomba vyombo vya dola vituangalie vitulinde, na kama hakuna ulinzi tujilinde wenyewe, kama mtu anakuja kuuawa hapa, maaskari wanakamata mtu badala wapite naye kwenye lami, wanapita naye nyuma kuja kumuulia sehemu kama hii, wananchi tuwaelewe vipi?  ninaomba serikali ya Magufuli kama kweli ni serikali ya wanyonge, muwatetee wanyonge kama hawa waliopata shida hapa”, amesema Mzee Suguta.

Ijumaa ya April 27, 2018, Kijana Chacha Heche Suguta aliuawa kwa kuchomwa kisu na polisi wa kituo cha Sirari Tarime, tukio ambalo limethibitishwa na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya Henry Mwaibambe, na kumshikilia polisi huyo aliyefanya mauaji.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad