Msanii wa muziki wa kizazi kipya Ben Pol amefunguka na kudai hakuna faida yeyote aliyoipata katika utoaji wa albamu na kuwataka mashabiki kuwa wazalendo katika kutoa ushirikiano kwa wasanii wanao wapenda ili mradi waweze kufika sehemu wanayostahiki.
Ben ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha eNewz kutoka EATV baada ya kuwepo upepo wa wasanii wengi kukimbilia kutoa albamu za muziki bila ya kufanya tathimini ya soka lilivyo kwa nyakati hizo.
"Bado ni changamoto kiukweli, kwasababu tukiongelea albamu yangu ya zamani 2011 mauzo yake yaliyonifikia mimi ni sawa sawa na 'show' moja ninayofanya. Hapa katikati ilikuwa shida ipo kwetu sisi wasanii hatutoi albamu lakini sasa hivi tunatoa na shida hizo zimehamia kwa watu, tunaomba watuunge mkono", amesema Ben Pol.
Pamoja na hayo, Ben Pol ameendelea kwa kusema "watu tunatakiwa tujifunze kuthamini vya kwetu na kuvipenda. Kama kweli unampenda Ben Pol basi unapaswa ununue 'CD' yake mwambie akusainie hata kama nyimbo hizo unazo nyumbani kwako. Ukinunua CD ni njia moja wapo ya kum-support msanii unayempenda".