Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Christian Bella amesema watu wa Kongo ni wabishi kumuelewa msaniii hususan akiwa anaimba kwa lugha tofauti na Lingala, ambayo wao ndio wanaitumia kwa asilimia kubwa.
“Kuna ugumu wa lugha, kule mara nyingi wanapenda Lingala ndio inapenya sana, kuna sehemu wanaongea Kiswahili, ambakoo ngoma za bongo zinahit vile vile, ugumu unapokuja ni wabishi sana, mpaka wakupitishe wakukubali, wabishi sana”, amesema Christian Bella.
Christian Bella amesema hata yeye kuweza kuanza kukubalika nchini kwao ni kutokana na Watanzania kumpokea na kumkubali, na kumfanya kuwa msanii mkubwa ndani na nje ya nchi.
“Kwa ugumu wote wa game ya Kongo na kutumia Kiswahili lakini nimepata nafasi, na hii ni kutokana na Watanzania wamenipa nafasi, wengine walikuwa wanashindwa kunitambua kama ni Mkongo au ni Mtanzania, unaweza ukawa unajua sana lakini watu wakakutaa, lakini ukifanya kikubwa nje, ndani wanakupokea”, amesema Christian Bella.
Hivi karibuni Christian Bella ameachia kazi yake mpya aliyomshirikisha Joh Makini, ikiwa ni si mara ya kwanza kwa wawili hawa kufanya kazi pamoja.