Baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuonyesha kuwa makusanyo ya serikali yanafikia lengo kwa takribani asilimia 94, lakini fedha za maendeleo zinazotolewa ni takribani asilimia 50 pekee Serikali imesema kwa mwezi inakusanya wastani wa Sh trilioni 1.3, Sh bilioni 550 hulipa mishahara na Sh bilioni 600 hulipa deni la taifa.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema hayo jana Alhamisi Aprili 12, wakati akizungumza na waandishi wa habari kujibu sehemu ya hoja zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Hesabu za Serikali (CAG), katika ripoti yake inayoishia Juni 2017 aliyoiwasilisha bungeni jana.
Dk. Mpango alisema; “kwa hiyo maana yake kwenye Sh trilioni 1.3, umebakiwa na bilioni 200 ambazo ndiyo hizo unatumia kuendesha Serikali, lakini humo namo kuna shughuli nyingine ambazo hazikwepeki, kwa mfano askari wetu shupavu wanalala nje lazima Serikali tuwape posho ya chakula, ndiyo sisi tunaweza tukaendelea na vurugu huku bungeni tukabishana, tukala nyumbani kwa amani.
“Kuna mishahara ya Majaji lazima ilipwe na marupurupu yao mengine, kuna viongozi wetu nao hawalali, niwahakikishie ni kawaida kabisa kumpigia Rais simu saa nane, saa tisa yuko macho, hawa viongozi wamebeba dhamana kubwa lazima Serikali iwahudumie.
“Kwa hiyo unaponiuliza hizi nyingine zinaenda wapi, naweza nikaendelea na kuendelea,” alisema Dk. Mpango.
Awali, Dk. Mpango alisema Serikali ya awamu ya nne, ilikuwa inakusanya Sh bilioni 850 kwa mwezi, lakini tangu Serikali ya awamu ya tano kuingia, imekuwa ikikusanya wastani wa Sh trilioni 1.
“Kwa hiyo ni ni rahisi sana kuhesabu hicho kinachoingia mfukoni, lakini ni muhimu kuangalia sana hicho kinachotoka, zinatoka zinakwenda kwenye nini.
“Ulipaji wa deni la taifa inategemea, kwa mwezi inaweza ikatoka kati ya Sh bilioni 600, tumewahi kwenda mpaka Sh bilioni 900, kutegemea na hayo madeni yanaiva wakati gani, mwezi huu unaweza ukalipa Sh bilioni 600 na kidogo, mwezi ujao ukalipa Sh bilioni 700, ni kwasababu ya tofauti ile mikopo inaiva wakati gani.
“Ukichukua wastani wa Sh bilioni 550 mishahara, ukaongeza Sh bilioni 600 kwaajili ya kulipa deni, tayari Sh trilioni 1.1 umeitumia kwa hivyo vitu viwili ambavyo huwezi kukwepa,” amesema Dk. Mpango.