Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga amesema, jalada la kesi ya aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini amelifunga rasmi.
Hayo ameyasema leo Aprili 20, 2018; Ikulu jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari huku akionya watu wanaovunjua amani kutofumbiwa macho wakiwamo waandishi wa habari.
Amesema jeshi la polisi linapotumia nguvu kuzuia maandamano, haliwezi kushtakiwa au hata kukitokea vurugu na kusababisha mauaji huwezi kulishtaki jeshi.
”Katika maandamano yale ya watu zaidi ya 200, huwezi kubaini nani amehusika na kumpiga risasi Akwilina na mwili wake haukutolewa risasi yoyote.”
Alipoulizwa kuhusu askari waliokamatwa baada ya kutokea kwa tukio hilo, Biswalo amesema, “kama jalada nimelifunga, kwa hiyo askari wale nao wameachiwa huru hawana hatia.”
Mkurugenzi huyo amesema moja ya jukumu lake ni kuhakikisha amani inakuwapo,”na niseme tu kuwa, mimi sina chama cha siasa, si mwanasiasa, kwa hiyo sitamvumilia mtu awe mkubwa wala mdogo, nitamshughulikia.”
“Na wanaosema wataandamana, waambieni wasifanye hivyo kwani wakiandamana watakwenda kuwasilimulia familia yake,” amesisitiza Biswalo
Pia, amevionya vyombo vya habari ambavyo vinavyoweza kuchangia uvunjifu wa amani, hatua zitachukuliwa hivyo kuvitaka kuwa makini na kutimiza wajibu wao kwa kufuata misingi ya taaluma yao.