Hali ya sintofahamu imeibuka katika familia ya marehemu Shehe Yahya Hussein na familia ya Idarusi, baada ya kujikuta wakigombea maiti ya mume wa binti wa Shehe Yahya aitwaye Mariam Yahaya Husein, baada ya ndugu wa mumewe huyo kumuwekea ngumu kushiriki mazishi.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha kuaminika ambaye yupo karibu na familia hiyo (hakupenda jina lake liandikwe gazetini), sakata hilo limefika pabaya kiasi kwamba mwili wa marehemu imebidi ushikiliwe na polisi mpaka pale watakapokubaliana nani azike.“Marehemu shehe Yahya ana binti aitwaye Mariam ni maarufu kwa jina la Mamu. Huyu alikuwa na mumewe aitwaye Idarusi na kwa pamoja wana watoto wawili.
“Huyo bwana kiukweli alikuwa na uwezo mzuri wa kifedha kwani aliwahi kufanya kazi Umoja wa Mataifa kama mtaalamu wa lugha na baada ya kustaafu alikuwa analipwa malipo mazuri tu ya kiinua mgongo.“Sasa kwa muda mrefu takribani miezi tisa huyo mumewe alikuwa anaumwa na Mariam, alikwenda naye India kwa ajili ya matibabu.“Huko, Mariam kahangaika naye kwelikweli lakini mwisho huyo mwanamme wiki iliyopita Aprili 5, alifariki dunia,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliendelea kueleza kwamba baada ya mumewe kufariki dunia, Mariam alirudi nchini na maiti ya mumewe kwa ajili ya taratibu za mazishi. Lakini alipofika shemeji zake walimwambia hatakiwi kufikia msibani badala yake anatakiwa kufikia hotelini, kwa hiyo akafikia Lamada.
Chanzo hicho kiliendelea kueleza kwamba akiwa hotelini hapo, ndugu wa marehemu walitaka kumzunguka ili waweze kuuchukua mwili na kuusafirisha mpaka Arusha kwa ajili ya mazishi.
“Si unajua tena mali za mirathi, mwenye cheti cha mazishi ndiye anaweza kufungua jalada la mirathi. Sasa michakato ya kubeba mwili kimyakimya ikiendelea na Mariam alitonywa.“Ikabidi aende uwanja wa ndege na kuzuia taratibu za kuchukua mwili kuendelea na kudai yeye ndiye ana haki ya kumzika mumewe kwani ndiye kamtoa India na amepata naye shida na si mtu mwingine.
“Hapo ndipo soo lilipoanzia na kutinga kwenye kituo cha polisi cha uwanjani hapo. Baadaye ndugu nao wakaamua kuibua suala lingine kwamba hawakubaliani na taarifa za msiba wa ndugu yao na wanahitaji mwili ufanyiwe uchunguzi, mwili ukachukuliwa na kupelekwa Muhimbili,” kilisema chanzo hicho.
Amani lilitinga nyumbani kwao Mariam, lakini pia halikuweza kumpata zaidi ya kukutana na kaka yake Mtabiri Maarufu nchini, Maalim Hassan Yahya Hussen ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.“Ni kweli mlichosikia. Mariam ni mdogo wangu baba mmoja na mumewe huyo Idarusi ninamfahamu maana alimuoa kwa ndoa miaka takribani sita na wameishi muda mrefu nyumbani kwetu Magomeni.
“Wana watoto wawili na wiki iliyopita huyo mumewe alifariki dunia. Sasa familia ya mwanaume inaonekana ilikuwa haina mazungumzo mazuri na huyu mdogo wangu, ndipo kizaazaa kilipoanzia, kila mmoja anataka amzike marehemu imefikia hatua mpaka upande wa mwanaume wanataka mwili ufanyiwe uchunguzi kwani hawana imani na taarifa za kifo chake.
“Binafsi nimeombwa kuliingilia hili suala, kwa hiyo nitajitahidi marehemu afanyiwe uchunguzi Muhimbili kisha azikwe kwanza halafu mambo mengine kama ni ya mali na nini zifuatwe sheria lakini marehemu akiwa amekwishazikwa,” alisema Maalimu Hassan.Upande wa Idarusi pia hawakupatikana kutoa ushirikiano licha ya kuwapigia simu ndugu zake waitwao Aikal na Hassan, simu zao zilikuwa hazipokelewi.
Afisa mmoja wa Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji alithibitisha kutokea kwa jambo hilo.