Vilevile, imesema mpaka sasa ujenzi wa reli hiyo kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) umepiga hatua saba.
Utekelezaji wa mradi huo unahusisha ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ambao sasa unaendelea kwa Dar es Salaam-Morogoro (km 205) na Morogoro-Makutupora (km 422).
Akiwasilisha bungeni mjini hapa jana hotuba yake kuhusu makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alisema hadi sasa ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam-Morogoro umefikia asilimia 10 na unatarajiwa kukamilika Novemba mwakani.
Akizungumzia hatua saba muhimu zilizofikiwa katika ujenzi wa reli hiyo, Prof. Mbarawa alisema hatua ya kwanza ya ujenzi wa kambi ya mkandarasi ya Dar es Salaam imekamilika kwa asilimia 99, Soga umekamilika kwa asilimia 89 na Ngerengere asilimia 67.
Alisema hatua ya upimaji wa ardhi itakakopita reli hiyo (topographical survey), umekamilika kwa asilimia 95.
Waziri huyo alisema hatua ya tatu iliyofikiwa ni njia ya kuhudumia mradi itakayotumika kupitishia watu, mitambo na vifaa vya ujenzi ambayo imekamilika kwa asilimia 83.
"Jumla ya vifaa kwa ajili ya ujenzi (mitambo na magari 755) vimeshawasili kwa ajili ya kazi. Kazi ya kusafisha eneo la mradi nayo imekamilika kwa asilimia 59.7," alisema.
Prof. Mbarawa alitaja hatua ya sita iliyofikiwa kuwa ni utafiti wa ardhi itakayobeba misingi ya madaraja pamoja na makalavati ya kuvukia watu, wanyama na baiskeli ambao umekamilika kwa asilimia 10.
Waziri huyo alisema hatua ya saba ni ujenzi wa tuta la reli ambayo imekamilika kwa asilimia 15.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa sehemu ya pili inayoanzia Morogoro hadi Makutupora yenye jumla ya urefu wa kilometa 422 (km 336 njia kuu na km 86 njia za kupishana treni) unaendelea vizuri.
"Mkataba wa ujenzi kwa utaratibu sanifu na jenga, ulisainiwa Septemba mwaka jana kati ya iliyokuwa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) na kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki," alisema na kusema zaidi:
"Mhandisi mshauri wa mradi huu ni muungano wa kampuni nane unaoongozwa na kampuni ya KORAIL ya Korea Kusini."
Alisema taratibu za kusaka fedha za ujenzi wa reli ya kisasa kwa maeneo ya Makutupora-Tabora (km 295), Tabora-Isaka (km 133), Isaka-Mwanza (km 250), Tabora-Uvinza-Kigoma na Kaliua-Mpanda-Karema zinaendelea.
"Nchi za China, Korea, Ujerumani, Ufaransa, India, Marekani, Nigeria, Ureno na Uingereza zimeonyesha nia ya kushiriki katika ujenzi huo," alisema.
"Zabuni kwa ajili ya kununua treni na mitambo itakayotumika kutoa huduma ya usafiri kwenye reli ya kisasa ilifungwa Februali, mwaka huu na tathmini inaendelea."
Jiwe la msingi la ujenzi wa sehemu ya reli hiyo liliwekwa na Rais John Magufuli, Machi 14, mwaka huu na ilielezwa kuwa unatarajiwa kukamilika Desemba 2020.
Prof. Mbarawa pia alisema serikali inatambua umuhimu wa reli ya kati iliyopo sasa kwa ajili ya kutoa huduma za mizigo na kuendelea kusafirisha mitambo na vifaa kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa inayojengwa.
Kwa kutambua umuhimu huo, alisema maandalizi ya kukarabati miundombinu ya reli ya kati kupitia Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Reli (TIRP) unaogharamiwa kwa fedha za mkopo kupitia Benki ya Dunia (WB), yanaendelea.
Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa alisema kuwa mwaka ujao wa fedha, Shirika la Ndege (ATCL) limetengewa Sh. bilioni 495.6 kwa ajili ya kununua ndege mbili; moja aina ya Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 76 na ndege kubwa ya masafa marefu aina ya Boeing 787-8 (Dreamliner) yenye uwezo wa kubeba abiria 262.
Prof. Mbarawa alisema fedha hizo pia zitatumika kulipia bima, gharama za uendeshaji wa ndege (start up cost), mafunzo ya marubani, wahandisi na wahudumu na ulipaji wa madeni.
Waziri huyo pia alisema kuwa katika mwaka ujao wa fedha, serikali itaendelea kuboresha huduma zinazotolewa na Shirika la Reli (TRC), Sh. trilioni 1.506 (fedha za ndani) zikitengwa.
Akifafanua kuhusu fungu hilo, Prof. Mbarawa alisema Sh. trilioni 1.4 zitatumika kuendelea na ujenzi wa reli ya kati (Dar - Morogoro km 300 na hadi Makutupora (km 422) kwa kiwango cha Standard Gauge.
Alisema Sh. bilioni 100 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli ya Isaka-Rusumo (km 371) kwa kushirikiana na Rwanda, Sh. bilioni tatu zimetengwa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na kumwajiri mtaalamu atakayeandaa nyaraka na kusaidia kutafuta fedha za ujenzi wa reli ya Mtwara-Mbambabay na matawi ya Mchuchuma na Liganga.
Prof. Mbarawa pia alisema kuwa katika mwaka ujao wa fedha, Sh. bilioni 9.29 ili kutekeleza miradi ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) ambayo ni pamoja na ununuzi na usimikaji wa rada nne za kuongozea ndege za kiraia katika viwanja vya JNIA, KIA, Mwanza na Songwe.
Aliongeza kuwa serikali imetenga Sh. bilioni sita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya sekta ya uchukuzi ikiwa ni pamoja na ununuzi wa magari ya zimamoto kwa viwanja vya ndege vya Mpanda, Shinyanga na Iringa.
Prof. Mbarawa aliliomba Bunge kuidhinisha jumla ya Sh. trilioni 4.271 ili kutekeleza majukumu yake kwa mwaka ujao wa fedha. Kati yake, Sh. trilioni 1.865 ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi, Sh. trilioni 2.387 za sekya ya uchukuzi na Sh. bilioni 18.856 za sekta ya mawasiliano.