Daraja la Nyerere, Kigamboni Dar es Salaam limeingiza Tsh. Bilioni 14.9 kwa kipindi cha July 2017 hadi March 2018.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa hivi karibuni kwenye mkutano mkuu
wa Baraza la wafanyakazi wa shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF),
makusanyo hayo ni wastani wa Sh. milioni 650 kwa mwezi. Makusanyo hayo
yametokana na wastani wa magari 10,393 yanayopita kwa siku.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema mafanikio
hayo yametokana na uamuzi wa kusimamia uendeshaji wa daraja hilo kwa
kutumia wafanyakazi wake.
“Kutokana na uwekezaji huo shirika linategemea kupata jumla ya Sh.
bilioni 14.53 zitakapoiva. Kwa maana hiyo mpaka sasa thamani ya
makusanyo ni sawa na shilingi bilioni 29.4,” alifafanua.
“Mtindo huu wa uendeshaji (kutumia wafanyakazi wa shirika) unatoa
uhakika wa kuendesha daraja kwa faida pamoja na kurudisha fedha za
wanachama,” alisema.
Daraja la Nyerere lenye urefu mita 680 lilizinduliwa Aprili 19, 2016
na Rais John Magufuli, ujenzi wake ulianza mwaka 2012 na kufanywa na
kampuni ya China Railway 15 Group ikishirikiana na kampuni ya China
Bridge Engineering Group ambapo ujenzi wake uligharamiwa na serikali kwa
asilimia 40 na NSSF kwa asilimia 60.