Hapa Ndipo Atakapozikwa Obama?

Hapa Ndipo Atakapozikwa Obama?
Marais saba wa Marekani na wake zao wamezikwa katika maeneo ya maktaba na makumbusho zilizobeba kazi zao za tangu ujanani hadi katika uongozi wa Taifa hilo.

Pia marais wote wa Taifa hilo wana utamaduni wa kutaja eneo watakalozikwa, kwa kuwa utangazaji hufanyika mara tu waingiapo Ikulu au wawapo katika mbio za kuwania kuingia Ikulu.

Hatua hiyo hufanyika ili kutoliweka Taifa katika sintofahamu pindi wanapoondoka duniani ghafla. Kwa sasa Marekani haina sheria ya eneo maalumu la mazishi ya viongozi kama zilivyo baadhi ya nchi zilizoendelea kutokana na kila mmoja kuwa na wosia wake tangu anapoanza maisha ya kujitegemea.

Hata hivyo, wakati huo ukiwa utamaduni wa kawaida wa marais hao kuwa na mahala wanapochagua kuzikwa washindapo uchaguzi kwa mara ya kwanza, Rais wa 44 wa Taifa hilo, Barack Obama hakufanya na hajafanya hivyo hadi sasa.

Maeneo walikozikwa marais wa Marekani yapo katika majimbo 23 ikiwemo District of Columbia. Marais 45 wameitawala nchi hiyo tangu mwaka 1789. Kati yao, 38 wamefariki dunia.

Jimbo lenye makaburi mengi walikozikwa marais ni Virginia walikozikwa saba. Tangu 1789, Wamarekani 49 wamehudumu kama makamu wa rais, kati yao 41 walishafariki dunia. Jimbo lenye makaburi mengi ya makamu wa rais ni New York walipozikwa 10.

Kizungumkuti cha Obama

Kwa upande wa Obama, inaelezwa kwamba hadi mwisho wa utawala wake ulioanza 2009 hadi 2017 hakueleza atazikwa wapi, iwe kwa maandishi au mdomo kwa wasaidizi wake.

Kwa wasaidizi na watu wake wa karibu ilibaki kuwa iwapo ingetokea akafariki dunia ghafla, basi angezikwa katika Jimbo la Chicago mahali ambako nyota yake ya kisiasa ilianzia kung’ara.

Hata hivyo, ikiwa ni zaidi ya miaka miwili sasa tangu astaafu, Obama yuko ‘bize’ na ujenzi wa makumbusho ya kazi zake ambayo pia itatumika kama maktaba katika eneo la Jackson Park, Chicago, mahala ambapo pia wengi wanadhani kaburi lake litajengwa hata kabla hajafa. Pia ni katika eneo hilo anapojenga makumbusho panatajwa kuwa ndipo mkewe, Michelle atakapozikwa. Marais saba wa Marekani na wake zao wamezikwa kwenye makumbusho au maktaba walizoanzisha, utaratibu ulioasisiwa mwaka 1945 baada ya kifo cha rais wa 32, Franklin Roosevelt.

Roosevelt alizikwa katika Makumbusho ya Taifa ya Historia ya Franklin Roosevelt iliyopo Hyde Park, New York.

Swali lililopo vichwani mwa wengi na ni Obama pekee mwenye jibu,

INAENDELEA UK 18

INATOKA UK 17

ni lile la mwanasiasa huyo aliyeondoka madarakani akiwa na miaka 55 atazikwa katika Jackson Park au wapi?

Taarifa za ndani zinadai makumbusho hiyo inayojengwa katika eneo la kati ya eka 23 hadi 24 haionyeshi kuwapo ramani ya kaburi au makaburi ya familia yake, ingawa kwa thamani ya ‘mjengo’ na ardhi vinavyofikia zaidi ya Dola 300 milioni za Marekani (zaidi ya Sh700 bilioni) lolote linaweza kufanyika iwe sasa au baadaye.

Baadhi ya wadadisi wa mambo wanasema utamaduni wa viongozi wa Taifa hilo kuzikwa katika makumbusho au maktaba zao umepitwa na wakati na kwamba, ni vyema kukawa na eneo maalumu la kihistoria litakalotumika kama sehemu ya makaburi ya marais walioitawala Marekani.

Hata hivyo, wanaopinga wana hoja kuwa makumbusho au maktaba zao kutengewa maeneo ya makaburi ni jambo jema na linavutia makumi kwa maelfu ya watu kuzitembelea ili kujionea vitu mbalimbali vilivyotunzwa.

“Palipo na kaburi kwenye maktaba ya rais, hilo ni jambo jema maana linavuta hisia za watu kufika na kujionea vitu vilivyomo,” anasema Benjamin Hufbauer, Profesa wa Chuo Kikuu cha Louisville ambaye pia ni mwandishi wa kitabu cha Presidential Temples: How Memorials and Libraries Shape Public Memory.

Profesa Hufbauer anasema, hata hivyo ni vyema Obama na familia yake wakazingatia kwamba kuweka eneo watakapozikwa katika maktaba hiyo ni jambo muhimu kwa sababu ya sifa tofauti alizonazo.

“Kwanza Obama alikuwa rais mweusi wa kwanza na pili, kizazi chake kina mchanganyiko wa uhamiaji na ukazi (wa Marekani) hivyo itakuwa vizuri zaidi akiwa na eneo hilo ambalo pia litawavuta mamilioni ya Waafrika na Wazungu kulitembelea,” anasema.

Marekani kuna maktaba na makumbusho 13 za marais, lakini ile ya Obama itakuwa chini ya Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka cha Taifa, ingawa kutokana na baadhi ya nyaraka alizotumia kama rais kuhifadhiwa maeneo tofauti haitapata fungu la fedha la kujiendesha kutoka kituo hicho. Kituo hicho ni idara ya Serikali.

Ingawa hadi sasa atakapozikwa Obama hapajafahamika, marais wanaoondoka madarakani wanatakiwa kiutaratibu kueleza watakapozikwa kwa mkuu majeshi kupitia kitengo cha huduma za wastaafu na zaidi ya hilo wanapaswa kupata ushauri wa kitalaamu, na hasa inapotokea kuwa sehemu hizo zinakuwa na masilahi mengi ya nchi.

Familia itaamua atakapozikwa

Kigingi kingine kinachoweza kuikabili makumbusho ya Obama ni kile cha iwapo ataamua kuwa eneo la makaburi liwepo ndani yake, sheria za Illinois zinataka kibali mpaka kitolewe baada ya usanifu mpya kuwasilishwa. Kwa sasa si Obama, taasisi yake wala makumbusho anayoijenga iliyowasilisha ombi hilo.

Licha ya kwamba rais huyo mstaafu hajafanya lolote mpaka sasa, na ukweli kwamba kifo hakipigi hodi, wanafamilia wataamua wapi watamfanyia maziko iwapo atafariki dunia kabla hajaamua atakapozikwa lakini vyovyote iwavyo mwili wake hautazikwa nje ya Chicago mahali ambako alikulia na kupatia umaarufu wake kisiasa.

Kwa mujibu wa watu wa karibu wa Obama, makumbusho yake inayotarajiwa kuzinduliwa miaka minne ijayo, itakuwa ya kisasa na yenye hadhi ya juu zaidi ikizingatiwa kwamba ndiye rais wa saba bora zaidi nchini humo (kwa mujibu wa utafiti wa mashirika makubwa matano ya habari nchini Marekani).

Marais 10 bora wa Marekani na ubora wao kwa mujibu wa mashirika hayo kwa kufuatia mtiririko ni Abraham Lincoln, George Washington, Franklin Roosevelt, Theodore Roosevelt, Thomas Jefferson, Harry Truman, Dwight Eisenhower, Obama, Ronald Reagan na Lyndon Johnson.

“Kama kutakuwa na eneo la makaburi nadhani litakuwa linatembelewa na watu wengi wakiwamo watalii kuona atapokuwa ‘amelala’ mmoja wa viongozi bora zaidi wa Marekani,” anasema mmoja wa wasaidizi wa Obama.

Mtendaji mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Makumbusho Afrika na Marekani iliyopo Charleston, Michael Boulware anasema utembeleaji wa maeneo ya kihistoria unamfanya mtu aguswe na historia husika.

“Unaweza kusikia hadithi popote, unaweza kuisoma kwenye vitabu viwili au vitatu, lakini kuwa katika eneo husika kunaongeza uwezo wa akili kujihisi ni sehemu ya historia,” anasema.

“Sidhani kama kuna swali kwamba Rais Obama hatakufa, lakini kama rais mwenye rekodi (zilizotukuka) na historia ya aina yake, anastahili kuenziwa na kadri muda unavyokwenda ataendelea kuonekana bora zaidi kihistoria.”

Obama pia anaweza kuamua kuzikwa katika Jimbo la Hawaii, huko ndiko alikozaliwa na kutumia muda mwingi wa ujana akilelewa na mama yake, Ann Dunham. Pia, Hawaii ndilo eneo maarufu kwa familia yake analolitembelea kila mara na pia Obama anaweza kuwa rais wa kwanza wa Marekani kwa mabaki ya mwili wake kuchomwa moto, utamaduni ambao unafanywa na jamii kubwa ya Kiasia nchini humo.

Walivyozikwa baadhi ya marais

Harry Truman alizikwa kwenye maktaba na makumbusho yake iliyopo eneo la Independence, Mo; Ronald Reagan alizikwa katika maktaba na makumbusho yake, Simi Valley, California; Herbert Hoover alizikwa kwenye maktaba na makumbusho yake West Branch na Dwight Eisenhower kwenye eneo la shughuli zake la Abilene lililopo Kansas.

Wengine ni Richard Nixon aliyezikwa kwenye viwanja vya maktaba ya rais vya Yorba Linda huko California na Gerald Ford aliyezikwa kwenye makumbusho yake ya Grand Rapids iliyopo Michigan.

Hata hivyo, John F. Kennedy na Lyndon Johnson hawakuzikwa kwenye maktaba na makumbusho zao zilizopo Boston na Austin. Kennedy aliyeuawa kwa risasi jijini Dallas, Texas, Novemba 22, 1963 alizikwa katika makaburi ya Arlington, ilhali Lyndon alizikwa kwenye ranchi ya familia iliyopo Texas.

Kati ya marais watano wa zamani wanaoishi, Jimmy Carter amekuwa akizungumza mara kwa mara juu ya mahala atakapozikwa akisisitiza kuwa lazima iwe katika mji aliozaliwa wa Plains uliopo Georgia. Maktaba na makumbusho yake ya kirais ipo Atlanta, mji ambao upo mbali na Georgia.

Oktoba, 2017 mtangulizi wa Obama, George W. Bush alitangaza kuwa yeye na mkewe Laura watazikwa kwenye makaburi ya Taifa ya Texas yaliyopo Austin. Baba yake, George H.W. Bush na mkewe Barbara wana eneo lao ndani ya maktaba na makumbusho ya kirais iliyopo Texas A&M University na tayari mkewe Barbara amezikwa katika eneo hilo Aprili 21 mwaka huu.

Kwa upande wa Bill Clinton na mkewe Hillary pia hawajatangaza watakapozikwa, lakini zipo fununu juu ya Washington kuwa ndio mji watakapozikwa na hawajakanusha taarifa hiyo.

Kauli za mabosi wa makumbusho

Mkurugenzi mtendaji wa maktaba na makumbusho ya Harry Truman, Kurt Graham anasema ukweli kwamba eneo hilo lina kumbukumbu nyingi za rais huyo wa zamani, lakini pia kuzikwa kwake hapo kunaamsha hisia zaidi za wageni wanaopatembelea, linaongeza umakini na tafakuri ambayo huwezi kuipata katika maonyesho yoyote duniani.

Truman alizikwa pembeni mwa kaburi la mkewe, Bess ndani ya maktaba hiyo na bintiye na mjukuu wake waliozikwa kando kidogo ya wawili hao.

Katika maktaba na makumbusho za akina Nixon na Reagan, wageni huyachukulia makaburi yao kama maeneo fulani ya matambiko, kukiwa na ukimya mkubwa wawapo sehemu hizo.

Msemaji wa Taasisi ya Reagan, Melissa Giller anasema: “ Sidhani kama wageni hawahisi hisia za ajabu kwa kuwa Rais Reagan na mkewe walizikwa hapa. Hapa wageni siku zote wako kwenye makaburi yao wakitoa heshima na baadhi yao pia huja na maua na kuyaacha juu ya makaburi haya.

Imekusanywa na Kulwa Magwa kwa msaada wa taarifa mbalimbali
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad