Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amefunguka na kuweka wazi kuwa endapo viongozi wa Chama Cha Wanasheria Nchini (TLS) watajiingiza kwenye masuala ya siasa na haraka hivyo wao hawataweza kushirikiana nao kwa kuwa sheria zinataka kutojihusisha na siasa.
Jaji Mkuu amesema hayo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari na kuwataka viongozi wa chama hicho kuendesha shughuli zao kwa manufaa ya Umma kwani ikiwa vinginevyo watakosa ushirikiano na vyombo vingine vilivyopo chini yake.
"Viongozi wanaoendesha chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) waendeshe gari lao kwa manufaa ya Umma wasikubali kuingia kwenye harakati na siasa kwani wakifanya hivyo wale ambao wanatakiwa kushirikiana nao hawatawapa ushirikiano, hivyo ukiingia kwenye siasa wengine sisi tumekatazwa kuingia kwenye mambo ya siasa hivyo hatutashirikiana na wewe" alisisitiza
Hata hivyo Rais wa Tanganyika Law Society (TLS), Bi. Fatma Karume akiwa kwenye kipindi cha East Africa Breakfast cha East Africa Radio aliweka wazi kuwa hana mpango wa kuingia kwenye siasa lakini amedai hawezi kuacha kuikosoa serikali pale anapoona inavunja sheria na kufanya mambo kinyume na kudai kwa hilo hataogopa kusema hata kidogo.
“I like my freedom, napenda kufanya vile ninavyoona mimi, kama serikali inafanya vitu kinyume na sheria nitasema kwamba hivi sio vizuri, si vizuri kuvunjia watu majumba yao wakati kuna court order, nitasema sitaogopa, ila sitaki kugombea, sitaki siasa, I like to be left alone”, amesema Fatma Karume.