Hii ndio Chanzo Uharibifu Mlima K’njaro

WANANCHI wanaozunguka Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), wamedaiwa kusababisha migogoro kati yao na hifadhi hiyo kutokana na kutofuata sheria na kanuni za hifadhi.

Akizungumza hivi karibuni na Nipashe, Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Pascal Shelutete, alisema chanzo cha migogoro ya mipaka husababishwa tafsiri zinazopingana kati ya wataalamu na wananchi kuhusu matangazo ya serikali yanayoanzisha hifadhi.

Shelutete alisema matatizo hayo yanaweza kuvuruga uhusiano kati ya wananchi na shirika na kutishia rasilimali zilizopo ndani ya hifadhi kupotea.

Alisema wamekuwa wakisisitiza wananchi umuhimu wa kuheshimu sheria ya mipaka za hifadhi za taifa, lakini ni changamoto kwa kuwa wananchi hawana uelewa wa kutosha.

Alisema watu wachache wenye nia mbaya wasipokemewa, madhara yatakuwa makubwa ikiwamo kupoteza uoto wa asili ambao ni chanzo cha utalii ndani ya hifadhi.

Hata hivyo, alisema TANAPA imeweka bikoni zenye viwango katika mipaka ya  hifadhi kwa  asilimia 80 na mwananchi atakayeingia eneo la hifadhi kwa kufanya shughuli za kibinadamu atachukuliwa hatua za kisheria.

Mkurugenzi wa TANAPA, Mtango Mtahiko, alisema migogoro mingi ya ardhi husababishwa na idadi ya watu kuongezeka huku akibainisha wakati wa uhuru kulikuwa na watu milioni nane na sasa wameongezeka hadi kufikia milioni 58.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zenye rasilimali za asili kama uoto wa asili, na maeneo ya kuzalisha mali yamepungua wakati binadamu wanaongezeka,” alisema Mtahiko.

Mhifadhi Mkuu KINAPA, Betrita Loibooki, alisema kutokana na uelewa mdogo wa wananchi wanaozunguka mlima Kilimanjaro, wanaona hakuna umuhimu wa kutunza misitu hivyo kulazimisha kuachiwa maeneo kwa ajili ya shughuli zao jambo ambalo ni hatari.

Alisema wananchi wanatakiwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa kwa kuwa faida zitokanazo na hifadhi hizo zinamfikia kila mwananchi na taifa.

Sheria ya TANAPA hairuhusu matumizi ya aina yoyote kasoro utalii wa kuangalia na kupiga picha, elimu na utafiti katika hifadhi za taifa.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Sikusona habari nzima, pale uliposema tatizo ni uelewa mdogo, umefanya intervention gani kuondoa hilo tatizo la uelewa mdogo? Sababu hatua kali haziondoi uelewa mdogo. Ingawa linaleta umaana wa kuwadhibiti wale watakaokaidi baada ya kupewa huo uelewa unaotakiwa.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad