Serikali imesema kutokana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 Tanzania inakadiriwa kuwa na watu zaidi milioni 44 lakini kati ya hao idadi ya wenye ulemavu ni zaidi ya milioni 2 sawa na asilimia 5.8 ya wananchi wote waliogawanyika katika makundi ya mbalimbali.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Mh.Stella Ikupa leo Aprili 11, 2018 kwenye kikao cha saba mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo linafanyika Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge Khadija Ali aliyetaka kujua iwapo serikali ina idadi kamili ya watu wenye ulemavu na aina ya ulemavu walionao na kusema aina ya walemavu waliyokuwa nao ni pamoja na ya watu wenye ualbino, kuona, kusikia, kutembea, kukumbuka, kujihudumia na ulemavu mwingine.
Mbali na hilo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Stella Ikupa amesema mtu yeyote atakayebainika kufanya vitendo vya ubakaji kwa watu wenye ulemavu atachukuliwa hatua kali za kisheria zinazostahiki dhidi yake.
Kwa upande wake naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama ametoa rai kwa watu wote na wawekezaji wanaoanzisha viwanda nchini Tanzania, kuwa watu wenye ulemavu nao wana nafasi ya kuongeza nguvu kazi ya nchi katika ujenzi wa taifa kupitia uchumi wa viwanda hivyo basi wapewe fursa kuzingatia sheria ya nchi.