Mchekeshaji maarufu, muigizaji na mshindi wa Shindano la Big Brother Afrika mwaka 2014, Idris Sultan amepata dili la kuwa balozi wa chapa ya kampuni ya usafiri ya Uber nchini.
Idris alitangazwa rasmi jana na kampuni hiyo ambapo Meneja Masoko wa Uber Kanda ya Afrika Mashariki, Elizaberth Njeri amesema kampuni hiyo ilifanya utafiti kwa miezi kadhaa ili kujua nani anawafaa, na Idris ameonekana sahihi kwao kutokana na mtindo wake wa maisha.
“Idris Sultan ni mcheshi, msanii ambaye hafanyi mambo yake kwa mazoea, pia anaheshimika katika tasnia ya uchekeshaji, tamthilia, na utangazaji wa vipindi vya redio. Tuna imani kwamba Idris atailetea Uber tija kubwa kwa sababu yeye anawasiliana na mashabiki wake kupitia mitandao ya jamii kila wakati,” amesema Njeri.
Kwa upande wake Idris ameshukuru kwa heshima aliyopewa na kusema amekubali kuwa balozi wa Uber si kwa kuwa amepata dili ambalo litamlipa, lakini yeye anaichukulia kama harakati ya kuwakomboa vijana wenzake katika changamoto ya ajira.
Amesema Uber isichukuliwe tu kama programu ya kutoa huduma ya usafiri bali ajira kwa vijana, hata wasomi hawatakiwi kuogopa kuwa washirika wa huduma hiyo kwa kuogopa kuitwa dereva.
“Kijana ambaye ana mawazo ya kutafuta, hapaswi kuwa na woga kwamba watu wengine watamchukuliaje bali kujali ni kiasi gani cha fedha kinaingia na maisha yako yanakwenda vipi,” amesema Sultan.
Meneja wa Uber nchini, Alfred Msemo amesema mchango wa Idris Sultan katika sanaa ya Tanzania unaendana na dhamira ya Uber ya kujenga kampuni ya kimataifa inayogusa maisha ya madereva na wasafiri wanaotumia mfumo huo nchini.