Mtoto wa miezi sita, Halfani Lema, mkazi wa Mtaa wa Ibanda Kata ya Nyegezi amefariki dunia saa chache baada ya mama yake kuachiwa kutoka Kituo cha Polisi Igogo, Nyegezi jambo ambalo limeibua utata.
Mama wa mtoto huyo, Ashura Theonest (26) alikamatwa na polisi Aprili 2, akidaiwa kuiba simu ya jirani yake hivyo kupelekwa mahabusu akiwa na mtoto wake.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Vedastus Mushola alisema jana kwamba mama huyo alipofikishwa kituoni hapo aliwaomba askari waliokuwa zamu ajidhamini ili arudi nyumbani kwani hakuwa na maziwa ya kumnyonyesha mwanaye usiku kucha lakini hakuruhusiwa.
“Pamoja na mwanamke huyo kueleza sababu hiyo, hakuna askari aliyemruhusu, lakini baadaye usiku hali ya mtoto ilibadilika na Aprili 3 mchana ndipo walimruhusu kwenda hospitali ya Wilaya Butimba kwa ajili ya matibabu,” alidai Mushola.
Mwenyekiti huyo alisema mtoto huyo alifariki dunia baada ya kufikishwa hospitali wakati akitibiwa jambo lililozua hasira kwa wakazi wa eneo hilo wakisema polisi ndiyo waliosababisha kifo hicho.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema si kweli kwamba polisi ndio waliosababisha kifo cha mtoto huyo akisema mama wa mtoto alijidhamini na kuruhusiwa kwenda nyumbani, “Yule mama alipofika nyumbani mtoto wake, aliumwa akampeleka hospitalini na alifia hospitali. Hizi taarifa za kwamba mtoto alifia kituoni si za kweli, kwanza kituo cha Igogo hakina mahabusu ya wanawake kuna mahabusu ya wanaume tu, kwa hiyo ukweli ndio huo.”
Mushola alilitaka jeshi la polisi kuwashirikisha wenyeviti wa mitaa husika pindi yanapotokea matukio kwenye mitaa yao ili kuepusha adha kama hizo, “Matukio madogomadogo yawe yanasuluhishwa kwenye uongozi wa mtaa, kwanza mimi nilikuwa sijui tukio hilo hatujashirikishwa mpaka linafika polisi.”
Ashura hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa sasa akieleza kuwa ana maumivu makali ya kupoteza mtoto wake lakini wananchi wenzake wa Mtaa wa Ibanda walisusia msiba huo wakitaka maelezo ya kina kutoka polisi.
Hali hiyo ililazimu maiti kukaa mochwari kwa siku tatu hadi pale uongozi wa polisi ulipotolea ufafanuzi suala hilo ndipo wananchi walipokubali kumzika mtoto huyo jana katika makaburi ya mtaa huo.
Ofisa utumishi wa Hospitali ya Nyamagana Andrew Chinduo alisema hakuwa na taarifa kuhusu tukio hilo lakini alitaka atafutwe Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba kwani ndiye msemaji mkuu.
Hata hivyo, Kibamba alipotafutwa simu yake iliita bila kupokewa.
Imeandikwa na Ngollo John, Jesse Mikofu na Sada Amir, (Mwanz