Rais wa zamani wa Malawi Joyce Banda anatarajiwa kurejea nyumbani Jumamosi baada ya kukimbilia uhamishoni alikoishi kwa zaidi ya miaka mitatu kwa sababu ya madai ya kuhusika katika rushwa, amesema msemaji wa chama chake.
Kashfa iliyofahamika kama Cashgate ni ufisadi ulioibuliwa ukiwahusisha maofisa wa ngazi ya juu kwamba walijichotea mamilioni ya dola kutoka hazina ya serikali na ulifichuka mwaka 2013 wakati akiwa rais.
Wahisani waliamua kukata misaada hali iliyozuia ukuaji wa maendeleo nchini Malawi, moja ya nchi masikini zinazotegemea sana misaada ya kigeni.
Banda, rais wa kwanza mwanamke nchini Malawi, aliangushwa katika uchaguzi mwaka 2014 na Rais Peter Mutharika aliyeshinda. Baada ya kuanza kushutumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka na utakatishaji fedha madai ambayo alikanusha, aliondoka nchini na hajarudi tangu hapo.
“Naweza kuthibitisha kwamba kama chama tumepokea mawasiliano kutoka ofisi ya rais wa zamani kwamba anarejea nchini Malawi Jumamosi,” alisema naibu msemaji wa chama cha PP, Ackson Kaliyile.
Julai mwaka jana polisi walitoa hati ya kumkamata Banda, wakisema shutuma za makosa yake ni sehemu ya Cashgate. Lakini mapema mwaka huu Taasisi ya Kupambana na Rushwa ilisema haikuwa na ushahidi wa kutosha kuusimamia dhidi yake, kwa namna fulani kama ikimsafisha mwanamama huyo.
Polisi hawajasema hadharani ikiwa mashtaka dhidi yake yametupwa. Msemaji wa polisi alisema Jumatatu kwamba polisi hawatatoa maoni yoyote kwa suala lolote hadi Banda awe amerejea nchini.
Mwaka 2016 Banda alitangaza akiwa uhamishoni kwamba atawania urais katika uchaguzi mkuu mwaka 2019, na chama kimesema anarudi kwa maandalizi hayo.