Kamati ya Bunge Yampa Rungu Msajili Kuvifutia Usajili Vyama vya Siasa

Kamati ya Bunge Yampa Rungu Msajili Kuvifutia Usajili  Vyama vya Siasa
Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa asisite kufuta usajili kwa chama chochote cha siasa kitakachokiuka sheria, kanuni na utaratibu wa uendeshaji wa vyama vya siasa nchini.

Pia, imeshauri ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ihakikishe kuna usimamizi wa karibu wa kuchunguza mienendo inayoharibu sifa na vigezo ya vyama vya siasa nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa alisema hayo bungeni jana alipowasilisha maoni ya kamati kuhusu hotuba ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu na ofisi ya Bunge kwa mwaka 2018/19.

Akiwasilisha maoni hayo baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kusoma hotuba yake, Mchengerwa alisema ofisi ya msajili ivifutie ruzuku vyama vitakavyobainika kutumia fedha kinyume cha madhumuni yaliyokusudiwa ili kutoa fundisho kwa vyama kuzingatia matumizi stahiki ya fedha za wananchi.

Kamati imeiagiza ofisi ya msajili kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa matumizi ya ruzuku kwa vyama vya siasa, hatua inayolenga kuhakikisha fedha zinatumika kama ilivyokusudiwa.

“Kamati inaishauri Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuzingatia sheria, kanuni, utaratibu na weledi katika usimamizi na utoaji wa ruzuku kwa vyama vya siasa,” alisema.Akizungumzia maoni ya kamati hiyo kuhusu vyama vya siasa, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema ushauri uliotolewa ni mzito, hivyo nakala ya taarifa ya kamati atapewa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Mchengerwa pia alizungumzia mgogoro ndani ya CUF na kusema kamati inashauri msajili kufanya jitihada za kutosha kuusuluhisha ili kuepusha athari kubwa zinazoweza kujitokeza katika Muungano.

CUF kwa muda mrefu sasa imekuwa katika mgogoro ulioigawa pande mbili; moja inayomuunga mkono katibu mkuu Maalim Seif Sharif Hamad na nyingine Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Mbali ya masuala hayo ya vyama vya siasa, Mchengerwa aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Bunge kuiwezesha kamati yake kufanya ukaguzi wa hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa makazi ya Waziri Mkuu ili kujiridhisha na ujenzi wake na kiasi cha fedha kilichotumika.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi

Kamati hiyo pia imeishauri Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ihakikishe inafuatilia wasimamizi wa uchaguzi na kuwawajibisha wanapofanya uzembe unaosababisha madhara ambayo yangeweza kudhibitiwa mapema na msimamizi aliye makini na anayetambua na kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

“Kamati inashauri tume kujitahidi kufanya kazi kwa weledi ili kuendelea kuaminika kwa wadau wa uchaguzi. Hii ni pamoja na kuhakikisha inawashirikisha wadau wakati wa uhuishaji wa daftari la wapiga kura ili kuepuka migogoro isiyokuwa na tija kwa Taifa,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, Oscar Mukasa akiwasilisha maoni kwa hotuba ya Waziri Mkuu alisema kamati yake inashauri Serikali kuipa fedha Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili iwe karibu na wananchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia alisema kamati maalumu zimekuwa zikiteuliwa kushughulikia mambo muhimu yenye masilahi ya kitaifa ambazo hazikutengewa bajeti kwa mwaka wa fedha husika hivyo kushauri Serikali ihakikishe inazirejesha mapema fedha zitakazotumika kutoka mfuko wa Bunge.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad