Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, amesema hakuna umuhimu mamlaka za serikali kutumia vyombo vya habari kuwaita baadhi ya watu kwa ajili ya kuwahoji kutokana na tuhuma wanazokabiliwa nazo.
Shabiby amesema hayo Bungeni Mjini Dodoma jana Aprili 12, 2018 huku akitolea mfano tukio la Mwenyekiti wa TSNP ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu (UDSM), Abdul Nondo, ambaye aliitwa na Mamlaka ya Uhamiaji kwa ajili ya kuhojiwa uraia wake, na kusema kwamba vitendo hivyo vinaichafua serikali kwa kiasi kikubwa.
“Sasa hivi kuna watu kwenye Utumishi ambao wanafanya mambo ya kuichafua Serikali ya CCM, kulikuwa na haja gani ya kumita yule kijana Abdul Nondo kumhoji sijui alete cheti cha kuzaliwa cha bibi cheti cha mjomba, cheti cha babu? Mamlaka inashindwaje kufanya investigations zake (uchunguzi) ili kubaini ukweli mapaka iite wanahabari?
“Tunawapa watu umaarufu wakati kesi ipo polisi, ipo mahakamani, kuna watu wengine watatumia hiyo kitu kusema Serikali ya CCM ikimtaka mtu inamuomba uraia wake, sidhani kama Serikali ina haja na mtu mdogo kama yule ambaye hata hana madhara yoyote,” alisema Shabiby.