Life Style ya Ommy Dimpoz Yaacha Maswali Mengi, Afananishwa na Warembo Kama Sanchoka

NI kijana flani hivi mtanashati, kipenzi cha kinadada, akicheka mashavuni anabonyea pia ana sauti nzuri anaposikika nyuma ya biti. Anamiliki Lebo ya PKP (Pozi Kwa Pozi) na wimbo wake wa Me and You ulibeba tuzo tatu katika kinyang’anyiro cha Tuzo za KTMA 2013.

 Bado hujamjua tu? Sikia tena, yupo chini ya Lebo ya Rockstar400, ni mzaliwa wa Kigoma, wimbo wake wa mwisho kutoa unaitwa Cheche na anapenda maisha ya bata!

Hapo je? Kama bado hujamjua sasa hapo utakuwa ‘slow’ mtu wangu, lakini sio kesi, ngoja nikutafunie umeze, ninamzungumzia mkali kwenye gemu la Muziki wa Bongo Fleva, Omari Nyembo ambaye anafahamika zaidi kwa jina la Ommy Dimpoz. Ommy ametengeneza hit kadhaa kwenye gemu la Bongo Fleva. Baadhi yake ni Nai Nai, Ndagushima na Baadaye.

Hata hivyo mbali na kupendwa na mashabiki kutokana na ngoma zake kali zenye kuburudisha, miaka ya hivi karibuni amevuna pia mashabiki wengi wanaofuatilia ‘life style’ yake ya maisha ya bata kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram.

 Ommy amekuwa akitupia picha akiwa maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo kwenye miji mikubwa kama London, Dubai, Sandton, Machester, New York na sehemu nyingine mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye viwanja vikubwa vya michezo na mahoteli mbalimbali. Sasa ukianza kutazama life style yake hii, kwa kile anachokitupia kwenye Instagram, unaweza kufananisha na namna wanavyoishi mastaa wengi wa kike wakiwemo Tunda na Sanchoka!

 Hata hivyo ni life style yake hiyo inayoacha maswali. Ukisoma komenti kwenye ukurasa wake wa Instagram, unaweza kuona watu wanavyokuwa wanamuuliza maswali kuhusu bata zake. Kwamba nani yupo nyuma ya bata hizo na jeuri ya pesa anaitoa wapi.

Wengine wanafika hatua ya kuandika kwamba kwa muziki na mafanikio aliyonayo kwenye gemu la muziki hayatoshi pekee kuishi namna anavyoishi. Bata linazidi kipato chake kinachojulikana labda kama ikiwa ana madili mengine ambayo anayafanya kimyakimya!

 Sasa kama si muziki wake, nini kinampa jeuri ya fedha kiasi cha kuponda raha kama anavyofanya? Maana anamiliki lebo pia anamsimamia mwanamuziki Nedy Music, vyote hiyo ni vitu vinavyohitaji kuongozwa na pesa. Ukweli ni kwamba maswali haya hatuwezi kukwepa kujiuliza kama wadau wa burudani!

Mikito NusuNusu, imemtafuta mara kadhaa Dimpoz ili kuweza kuzungumzia bata zake lakini hajatoa ushirikiano, kwani ametumiwa sms, hajajibu, amepigiwa simu, hajapokea na gazeti limekwenda mpaka nyumbani kwake lakini halijafanikiwa kumpata. Hata hivyo, Dimpoz anafahamu kwamba mashabiki wake wana kiu ya kufahamu juu ya safari zake za nje na bata zake anapata jeuri wapi.

 Kwani hata hivi karibuni akizungumza na mtandao mmoja wa burudani amesema mashabiki wasijiulize sana kuhusu safari zake za nje kwani yupo bize nje kutokana na mambo ya kikazi kwamba toka asaini Rockstar400, ametakiwa kuandaa albamu. Kwa hiyo yupo bize kusafiri huku na kule kwa ajili ya kolabo. Lakini maswali ya kujiuliza, Old Traford anakwenda kufanya kolabo? Au mahotelini anakoonekana nako kuna kolabo?

 Kama ni kolabo mbona hatuoni picha za studio yupo ‘booth’ akiandaa kazi au yupo na msanii yeyote wa nje akiandaa mzigo mpya? Ipo wazi kwamba bado kuna maswali mengi ya kujiuliza. Ni vyema Dimpoz akaibuka na kukubali kutoa ushirikiano ili kukata kiu ya mashabiki wake ambao wamekuwa wakijiuliza maswali juu ya bata zake.

MAKALA: BONIPHACE NGUMIJE

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad