Kikosi cha Simba kimeshindwa kupata alama tatu na badala yake kimepoteza pointi mbili katika Uwanja wa Samora mjini Iringa dhidi ya Lipuli, mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Mchezo huo ulioanza kwa kasi zaidi kwa wenyeji wakionesha kuumiliki mpira zaidi ya Simba, walikuwa wa kwanza kujiandikia bao mnamo dakika ya 31 ya kipindi cha kwanza kupitia Adam Salamba.
Bao lilidumu kipindi cha kwanza ambapo mpaka Mwamuzi anapuliza kipyenga kwenda mapumziko, Lipuli walikuwa mbele kwa bao moja.
Kipindi cha pili Simba walijitahidi kuamka na kuanza kujibu mapigo baada ya Kocha, Pierre Lechantre kufanya mabadiliko ya kumtoa beki Juuko Murushid, na nafasi yake ikichukuliwa na Mshambuliaji, Mburundi, Laudit Mavugo.
Simba ilifanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 66 ya kipindi cha pili baada ya mpira wa kona kumfikia Mavugo ambaye aliumalizia kwa mguu na kufanya matokeo mpaka dakika 90 zinamalizika yaende sare ya 1-1.
Matokeo hayo yameipa Simba alama moja na kuifanya ifikishe pointi 59 kwenye msimamo wa ligi.