KOCHA Mzambia, George Lwandamina ameondoka leo kwenda Zambia na habari zinasema anarejea Zesco United ya kwao na atatambulishwa Alhamisi.
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amsema leo kwamba Lwandamina hajatokea mazoezini leo asubuhi bila sababu na wanamtafuta hapatikani.
“Mimi sijui kaenda wapi, kwa sababu hajaniaga. Hizo hizo habari (za kwenda Zambia) wewe ndiyo unaniambia,”amesema Mkwasa baada ya kuulizwa na Bin Zubeiry Sports – Online juu ya kocha huyo kurejea kwao, Zambia.
Habari zinasema kwamba Zesco United imeamua kumrejesha kocha wake huyo baada ya mafanikio yake Tanzania ndani ya miaka miwili, akiiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita na sasa inakaeribia kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga SC imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wolaita Ditcha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua hiyo Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo uliotokana na mabao ya Raphael Daudi kipindi cha kwanza na Emmanuel Martin kipindi cha pili, unamaanisha Yanga SC watahitaji kwenda kulazimisha sare ugenini wiki ijayo, au kutofungwa zaidi ya tofauti ya bao moja ili kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya pili baada ya mwaka 2016.
Na Lwandamina ambaye mkataba wake unamalizika Juni mwaka huu, anaondoka Yanga siku moja kabla ya kuteremka uwanjani kumenyana na Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Lwandamina alijiunga na Yanga Novemba mwaka 2016 akichukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm na katika kipindi hicho ameiongoza timu katika michezo 77 ya mashindano yote akitoa sare 18, kushinda 45 kati ya hizo mbili kwa penalti baada ya sare ndani ya muda wa kawaida na kufungwa 14, tano kwa penalti baada ya sare katika muda wa kawaida.