Mambo Yatakayokusaidia Kudumisha Mahusiano ya Mapenzi


Kuna nukuu inayosema “Uhusiano mzuri hautokei tu peke yake bali huchukua muda, uvumilivu, na watu wawili ambao kikweli wanataka kuwa pamoja.”

Japo inasemwa kuwa mapenzi hayana njia moja ya kufuatwa lakini kuna vitu ambavyo vinajulikana kuchangia katika kuboresha mahusiano baina ya wapenzi.

Mahusiano ya mapenzi yenye kudumu ni sharti yapandwe katika udongo wenye rutuba kama ulivyo mmea, yatahitaji maji ya kumwagilia na mbolea ya kukuzia.  Na zaidi ya yote yanahitaji muda wa kukua kabla matunda kuonekana.

1. Uaminifu
Kumwamini mwenza wako ni jambo la msingi sana katika kudumisha mahusiano. Usimshuku mpenzi wako kuwa si muaminifu bila ushahidi wowote. Kushukiwa kukosa uaminifu pasipo ukweli inasononesha sana na kumkosesha raha mpenzi wako.

Imesemwa na wanafalsafa wa mawazo ya binadamu kuwa “Unachofikiri na kuamini kinatokea” hivyo unashauriwa kutofikiri vibaya juu ya mpenzi wako kwani haileti afya katika mahusiano. Hali kadhalika na wewe uwe mwaminifu na mwenye kusema kweli mara zote. Ongeeni juu ya mipango na mawazo yenu bila kufichana.

Watambulishe kwa mpenzi wako ndugu ,jamaa na marafiki wakaribu ili kumpa mwenza wako amani.

2. Weka muda kwajili ya Mwenza wako
Mahusiano mazuri kati ya wapenzi yanahitaji muda wa wapenzi hao kukaa pamoja. Wapenzi wasio na muda wa kukaa wana hatari ya kupoteza mvuto wa mahusiano yao na hivyo kuhatarisha uhai wa mapenzi kati yao.

Kama wapenzi wapo mbali mbali basi wanahitaji kuweka muda wa kuongea kila inapowezekana. Tafuta muda wa kutoka pamoja, hata kama mtaenda mgahawani kunywa chai au juisi tu inatosha sana na inawaweka karibu zaidi.

3. Mawasiliano
Mawasiliano ni muhimu sana baina ya wapenzi. Hata kama umebanwa na kazi pata dakika chache za kuongea na mpezi wako na kumtaka hali. Andika hata ujumbe wa maneno au barua pepe. Mwambie mpenzi wako ulipo kila mara inapobidi ili kumjengea imani na wewe na kumpa amani moyoni. Tuma ramani ya mahali ulipo kama unatumia simu ya “Smart” (Tuma location kwenye whatsapp)
Mawasiliano ni ufunguo wa kudumisha upendo.

Wakati kuwasiliana na mpendwa wako, kumbuka kwamba upendo ni muhimu. Ongea toka moyoni na si kwa ajili ya kutimiza wajibu tu, kwani mpezi wako atajua tu kama hakuna mahaba katika mawasiliano yenu hivyo kutoleta faida ile inayotegemewa.

Mawasiliano mengine ni yale ya kuelezana yaliyo moyoni. Mweleze mwenza wako linalokusibu ili kupata ufumbuzi wa pamoja. Wapenzi wanaoongea kwa utulivu siku zote watakuwa pamoja.

4. Zawadi
Tafuta kitu cha kumpa mpenzi wako. Si lazima kiwe na thamani kubwa. Inaweza ikawa pipi au matunda tu. Mnunulie zawadi kila inapowezekana hasa unaposafiri au katika siku yake ya kuzaliwa.

5. Onyesha Upendo Wako 
Kila mtu anajinsi yake tofauti ya kuonyesha upendo, lakini vyovyote itavyokuwa ni jambo la muhimu sana kuonyesha hisia zako kwa mpenzi wako. Mara nyingi wapenzi wa muda mrefu wanasahau juu ya hili.

Maneno kama “Nakupenda”au majina ya mahaba kama “Mpenzi” au ”La-azizi” yanachangia sana kuonyesha mapenzi na kumfanya mwenza wako kujisikia vizuri. Maneno haya yanaposemwa kwa hisia halisi na toka moyoni yana mchango mkubwa katika kuboresha mahusiano.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad