Masaa kadhaa baada ya klabu ya soka ya Yanga kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la shirikisho nchini ASFC, Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye ni shabiki mkubwa wa Simba ametupa kijembe kwa watani wao Yanga.
Yanga jana jioni iliondolewa katika michuano hiyo na Singida United kwa jumla ya penalti 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Katika mikwaju ya Penalti kiungo wa Yanga Papy Tshishimbi alipaisha juu kitendo ambacho kimemfanya Mh. Zitto kutoa tahadhari hiyo.
''Tahadhari kwenu wananchi wa kondoa na vijiji vyake.. lile shuti la penalti ya shishimbi bado lipo hewani hivyo muwe makini na utuaji wake usijeleta madhara makubwa'', umesomeka ujumbe wa Zitto kupitia mtandao wa Twitter.
Mbali na Tshishimbi mchezaji mwingine ambaye alikosa penalti ni Emmanuel Martin huku Singida United wakipata Penalti zao 4 kati ya 5 na kuwafanya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ambayo hutoa mwakilishi wa Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Timu 4 ambazo zimefuzu hatua ya nusu fainali ni Stand United iliyoitoa Njombe Mji, JKT Tanzania iliyoitoa Tanzania Prison, Mtibwa Sugar iliyoitoa Azam FC na Singida United iliyoitoa Yanga SC.