Marekani, Ufaransa na Uingereza zimefanya shambulizi nchini Syria kumuadhibu rais wa nchi hiyo, Bashar al-Assad kwa shambulio la silaha za sumu dhidi ya raia na kuzuia kufanya hivyo tena.
Televisheni ya taifa nchini Syria imeripoti kuwamba vifaa vya ulinzi wa anga vya Syria, vilijibu shambulio hilo baada ya shambulio la Marekani na washirika wake kutulia.
Hatua hiyo ilijiri kufuatia tuhuma kwamba utawala wa rais Bashar al-Assad wa Syria, ulitumia gesi ya sumu kuwashambulia na kuwaua raia wake, wakiwemo watoto wachanga.
Katika hotuba yake kutoka White House jana Ijumaa mwendo wa saa tatu usiku saa za ukanda wa wa Mashariki mwa Marekani, Rais Trump alisema kuwa nchi hizo tatu zimeamua kuchukua hatua hiyo kama njia ya kuzima uwezekano ya mashambulizi mengine ya kutumia gesi ya sumu.
"Muda mfupi uliopita nimeamuru jeshi la Marekani kushambulia maeneo yaliyohusika na shambulizi la silaha za kemikali lililotekelezwa na utawala wa Bashar al-Assad," alisema Trump.
"Hatutakubali mashambulizi ya kemikali," aliongeza.
Trump aidha alilizishutumu Urusi na Iran kwa kile alichokiita "kushirikiana na uongozi wa Syria kufanya mashambulizi kwa raia wa Syria ambayo hayakubaliki."
Na akihutubia waandishi wa habari kwenye makao makuu ya kijeshi ya Marekani, Pentagon, waziri wa ulinzi Jenerali Jim Mattis alitoa maelezo zaidi kuhusu mashambulizi hayo, na kusema kuwa yalilenga vituo vitatu, kikiwemo kimoja cha utafiti na kingine cha kuhifadhi gesi ya sumu.
"Mashambulizi hayo ni makubwa zaidi ya mara mbili na yale tuliyoyafanya nchini Syria mwaka jana...na ni makubwa," alisema Mattis.
Kituo cha televisheni cha CNN kiliripoti Ijumaa usiku kwamba milipuko mikubwa ilisikika mjini Damascus punde baada ya rais Trump kutoa hotuba yake.
Katika hotuba yake, Trump aidha alieleza masikitiko yake kwamba licha ya rais wa Urus Vladmir Putin kuahidi kuchukua hatua za kuangamiza uwezo wa Syria wa kutumia silaha za kemikali, Russia bado haijafanya hivyo.
"Ni sharti Urusi iamue kama itaendelea kwenye barabara hiyo au itajiunga na nchi zinazotafuta amani," alisema rais huyo.