WAKATI homa ya mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga ikizidi kupamba moto, uongozi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kwa kushirikiana na Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) umekumbana na changamoto kubwa kuhusiana na mwamuzi atakayechezesha mechi ya watani hao wa jadi itakayofanyika Aprili 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Changamoto hiyo inatokana na mwamuzi aliyekuwa amepangwa kuchezesha mchezo huo hapo awali kukumbana na kashfa ya kuboronga katika mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Mbeya City na Yanga iliyofanyika hivi karibuni kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Mwamuzi wa mechi hiyo alikuwa ni Shomary Lawi kutoka Kigoma ambaye anadaiwa kushindwa kuumudu mchezo huo kutokana na kukosa umakini baada ya kuruhusu mchezaji aliyekuwa amefanyiwa mabadiliko kuingia tena uwanjani na kuendelea na mchezo.
Habari za kuaminika ambazo Championi Jumatano limezipata kutoka ndani ya TFF zimedai kutokana na Lawi kuboronga kwake katika mchezo wa Mbeya City na Yanga, uongozi wa Bodi ya Ligi pamoja na Kamati ya Waamuzi ya TFF, unaangalia ni cha kufanya kuhusiana na mwamuzi huyo, kama ataachwa achezeshe mechi hiyo au aondolewe na nafasi yake ichukuliwe na mwamuzi mwingine.
Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura ili aweze kuzungumzia hilo hakupatikana.