Mbunge Aitaka Serikali Kufuta Mfumo wa Vyama Vingi

Mbunge Aitaka Serikali Kufuta Mfumo wa Vyama Vingi
Mbunge wa Viti Maalum Chadema, Cecilia Pareso amesema kama serikali ina lengo la kuwabana na kuwanyima haki wapinzani, basi ni bora mfumo wa vyama vingi ukafutwa ili ifahamike kwamba nchi ni ya chama kimoja.



Pareso ameyasema hayo jana Aprili 5, Bungeni Mjini Dodoma wakati akichangia katika Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2018/19 huku akidai kwamba vyama vya upinzani vimekuwa vikionewa ikiwemo viongozi wake kukamatwa mara kwa mara na kufunguliwa mashtaka huku wengine wakifungwa jela. Amesema vyama hivyo vimekuwa ni adui mwingine kwa kuwa kwa sasa vinapigwa vita na Serikali iliyopo madarakani, kuzuiwa kufanya shughuli za siasa majukwaani.



Pia alidai chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni, zilikuwa ni kati ya Chadema na Jeshi la Polisi na kudai kwamba wabunge na madiwani walinunuliwa, wakahama vyama vyao, hivyo kukalazimika kufanyika chaguzi nyingine ndogo alizodai zimegharimu zaidi ya Sh bilioni 6.



“Kama mnakataza vyama vya siasa visifanye mikutano ya hadhara, hamuwezi kuja bungeni na kutueleza vyama hivi vimeendelea kufanya vizuri miaka 26 iliyopita. Enzui za Mwalimu Nyerere maadui wa nchi hii walikuwa watatu ambao ni umaskini, ujinga na maradhi, lakini kwa yanayoendelea, leo adui mwingine ni vyama vya siasa,” alisema Pareso.



Hata hivyo, madai ya Pareso yalipingwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Mwigulu Nchemba.



“Nataka kuwashauri wabunge, tunapoongelea taasisi ambazo zipo kikatiba, zinafanya kazi kwa ajili ya wananchi, tuheshimu kazi zinazofanywa. Uhalifu wowote unaofanyika ndani ya nchi, iwe wakati wa uchaguzi au wakati si wa uchaguzi, unahitaji kuwahakikishia raia usalama wao.



“Kuna uchaguzi mmoja chama chako (Chadema) hakikushiriki, hakukuwapo na matukio ya yoyote. Sisi kama Jeshi la Polisi tupo kwa ajili ya kuwahakikishia wananchi usalama, wala hatuwezi kuacha wananchi wakakatana mapanga na kuuwana,” alisema Mwigulu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad