Mbunge wa viti Maalum CUF Rukia Kassim Ahmed, ameibua hoja bungeni kutaka serikali iweke sheria ya kuhasi wanaume watakaobainika na makosa ya ubakaji wa watoto wadogo.
Mh. Rukia Ahmed ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akiuliza swali Bungeni kwa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto, akitaka kujua hatua stahiki wanazochukuliwa watu wanaofanya vitendo vya ubakaji kwa watoto, kwani zilizopo anaona ni ndogo hivyo zinachangia kuongezeka kwa vitendo hivyo.
“Kwa kuwa serikali inachukua hatua za kutosha dhidi ya udhalilishaji huu, lakini bado vitendo hivi vinaendelea kwa kasi kubwa katika jamii zetu, je, serikali haioni kwamba adhabu inayotolewa ni ndogo, hivyo basi, iletwe sheria hapa Bungeni tuipitishe, yeyote atakayepatikana na hatia ya kubaka mtoto mdogo ahasiwe?”, amesema Mbunge huyo.
Licha ya hilo Naibu Waziri wa Afya Faustine Ndugulile alijibu swali hilo akisema kwamba serikali inatambua vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto, na ndio maana ikatunga sheria za watoto ili kuwalinda.