Mbunge wa Viti Maluum (Chadema), Lucy Magereli amesema uamuzi wa Rais John Magufuli kununua ndege hauwezi kuwa sababu ya kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Akizungumza katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwaka 2018/19, mbunge huyo amesema kuliko kununua ndege hizo, Serikali ingekodisha ndege na kuanza kujipanga taratibu kuliboresha shirika hilo.
“Nani aliyemshauri Rais kununua ndege? Tungeweza kuifufua ATCL kwa ndege za kukodi, hatuhitaji ndege kubwa. Hivi tunawezaje kushindana na mashirika makubwa ya ndege duniani ambayo yapo muda mrefu na yamejiimarisha,” amesema.
“Suala si kuhitaji ndege, suala tumezipata kwa utaratibu upi. Tuna ndege wakati viwanja vya ndege vya ndani havifai kwa matumizi yetu. Leo mtalii akitua Dar es Salaam akitaka kwenda maeneo mengine atafika kwa shida.”
Mbunge huyo alihoji sababu za Serikali kununua ndege kubwa wakati haijaimarisha miundombinu, vikiwemo viwanja vya ndege, “ndege tunazonunua ni mzigo kwa nchi hii, zinahitaji matengenezo, tutayaweza?”
“Kesho na keshokutwa Bunge litakaa tena na kusema tumetumia fedha nyingi kuifufua ATCL na kuliingiza Taifa katika matatizo. Nawaambieni tutakaa hapa kujadili tena jambo hili.”
“Tumetumia fedha nyingi kukomboa ndege zetu zilizozuiwa Canada je hizo fedha Bunge gani limezipitisha?” Amehoji.