Meli Iliyokamatwa ni ya Serikali na Ilikua Ipo Kwenye Doria- Polisi

Meli Iliyokamatwa ni ya Serikali na Ilikua Ipo Kwenye Doria- Polisi
Jeshi la Polisi mkoani hapa limesema, meli inayodaiwa kuteka mashua na kisha ‘kutelekeza’ abiria Tanga, ni ya Serikali na ilikuwa ikifanya doria katika Bahari ya Hindi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema hayo jana wakati akifafanua tukio la abiria 54 kutelekezwa nje ya jengo la kikosi cha majini cha Jeshi la Polisi.

Alisema meli hiyo haikuwateka bali iliwakamata abiria hao kwa kuwa mashua waliyokuwa wakisafiria, haikusajiliwa kubeba abiria na ilikuwa imejaza kuliko uwezo wake.

Mashua hiyo inayodaiwa kutekwa ilikuwa na hao abiria wakitokea Shimoni, Mombasa, kuelekea Pemba.

“Maofisa waliokuwa ndani ya meli ya doria ya vyombo vya ulinzi na usalama waliamua kuizuia mashua iliyokuwa ikiwasafirisha abiria hao baada ya kubaini kuwa haikusajiliwa kuchukua abiria na ilijaza kupita kiasi ndipo wakaamua kuwaleta sehemu salama,” alisema Kamanda Bukombe.

Alifafanua kuwa kutokana na hali hiyo, Serikali imewaandalia basi maalumu litakalowasafirisha hadi jijini Dar es Salaam ambako watapanda boti ya abiria kuwapeleka kisiwani Pemba kupitia Unguja.

Wakizungumza na Mwananchi jana, abiria hao walisema baada ya kufikishwa nje ya Jengo la Polisi Marine, maofisa wa idara ya uhamiaji walichukua pasipoti zao za kusafiria kwa ajili ya uchunguzi na baadaye waliwarejeshea.

“Maofisa wa idara ya uhamiaji walikuja kuchukua paspoti zetu wakaenda nazo ofisini kwao lakini baadaye wakuatwambia hatuna matatizo,” alisema Time Bakari.

Abiria hao walilalamika kwamba maofisa wa meli hiyo ya Serikali waliwanyang’anya majaketi ya kujiokolea majini na hawakuwarejeshea.

Walisema viongozi wa Serikali walifika kituoni kuwaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza na kwamba tukio hilo limefanyika ikiwa ni jitihada za vyombo vya dola kuhakikisha Bahari ya Hindi eneo la Tanzania inakuwa salama.Polisi:
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad