Meli zakwama Bandarini Kutokana na Utata wa Kodi

KAMATI ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira imesema meli mbili za mafuta ghafi zimekwama katika bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya wiki mbili sasa kutokana na utata wa kodi inayotakiwa kulipwa.

Kufuatia hali hiyo, Serikali imeagizwa kulitafutia ufumbuzi suala hilo kwa kuwa linaweza kusababisha uhaba wa bidhaa zingine zinazotokana na mafuta hayo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Suleiman Sadiq Murad, katika semina ya kuwajengea uwezo wabunge kuhusu utendaji kazi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na Tume ya Ushindani (FCC).

Murad alisema kuna meli mbili zipo bandarini zimeleta mafuta hayo na kwamba Mkemia Mkuu, TBS wametoa cheti) kwamba ni ‘mafuta ghafi, lakini Mamlaka ya Mapato (TRA) imekataa, ikisema sio mafuta ghafi.

“Meli zile zimekaa bandarini, kwa sasa zina zaidi ya wiki mbili, meli moja ina tani 30,000 na nyingine ina tani 31,000,” alisema.

“Sasa katika hali kama hii inapotokea jambo la namna hii hivi kuna mawasiliano gani kati ya TBS na TRA kuhakikisha kwamba mizigo ile ambayo nyinyi wenyewe mmekagua na mnasema mzigo huu ni Crude Oil (mafuta ghafi) wakati TRA inasema Semi-Refined (yaliyosafishwa kidogo)?” alihoji Mwenyekiti huyo.

Alitoa tahadhari kwa serikali kuwa mafuta ya kula yameanza kupanda bei kwa sababu mafuta ghafi yaliyoko nchini yanatumika na viwanda havitakuwa na malighafi tena ya mafuta ghafi.

“Bunge limepitisha crude oil itatozwa asilimia 10 na semi- refined asilimia 25 sasa yule wa TBS anasema hii ni crude ilipiwe asilimia 10, TRA anasema ilipiwe asilimia 25,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema kuna tatizo na lipo bandarini na kumuomba Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, aliyekuwapo katika kikao hicho kwenda kulitafutia ufumbuzi.

“Naibu naomba ulichukue na mimi nitakaa na Kamati tuzungumze kwa kina kwa kuwa sisi tuna wajibu wa kushauri na kuisaidia serikali,” alisema.

“Eneo hili lina utata kidogo, tunaomba muangalie mnawezaje kulitatua kwa kuwa meli hizo mbili pale zinashindwa kushusha mafuta kwa sababu wenye viwanda, TBS wanasema ni crude, lakini TRA wanasema ni semi refined, tunaomba serikali isaidie suala hili,” alisisitiza Murad.

Akizungumzia suala hilo, Manyanya alisema suala la uagizaji mafuta lina uhusiano mkubwa sana na masuala ya kiuchumi katika nchi.

“Kwa vyovyote vile inapotokea jambo kama hili ngazi za maamuzi za juu zitakaa pamoja na kufikia muafaka namna gani ya kulishughulikia kwa manufaa mapana ya nchi yetu,” alisema Manyanya.

Awali, akitoa mada Kaimu Mkurugenzi wa TBS, Tumaini Mtitu, alisema shirika hilo linakabiliwa na upungufu wa vifaa vya kupimia bidhaa kwa sababu ya ufinyu wa nafasi ya maabara 24 na gharama ya kuvinunua.

“Pia kuna changamoto ya uelewa mdogo wa umma na jumuiya ya wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa viwango katika kulinda afya na usalama wa walaji na kuongeza uwezo wa kuuza bidhaa zetu nje ya nchi kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu,” alisema.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Dk. John Mduma, alisema Tume imefanikiwa kukamata na kuteketeza bidhaa bandia za aina mbalimbali zenye thamani ya Sh. bilioni 26 na ziliteketezwa kwa kuzingatia sheria husika na kanuni zake pamoja na taratibu za ulinzi na mazingira.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad