Mbunge wa Bariadi na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge amefunguka na kusema kuwa zaidi ya miaka 40 ya uhuru wa nchi serikali imekuwa ikishikilia eneo lenye ukubwa wa ekari 2,472 bila kulifanyia jambo lolote lile la maana na kuomba serikali iwarudishie wananchi ili waweze kulitumia eneo.
Chenge amesema hayo leo bungeni April 19, 2018 alipokuwa akihoji kama serikali ipo tayari kurejesha maeneo hayo ambayo hayatumiki kikamilifu kwa wananchi ili wananchi waweze kufanyia shughuli zingine, lakini Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alifunguka na kusema kuwa serikali haipo tayari kurudisha maeneo hayo kwa kuwa serikali iliyachukua kwa lengo magereza kuweza kuendesha shughuli za uelimishaji wa wafungwa kwa njia ya kilimo na ufugaji kupitia maeneo hayo.
"Gereza la Matongo lililopo mkoani Simiyu katika wilaya ya Bariadi lenye ukubwa wa ekari 2472 lilianzishwa mwaka 1975, baada ya kuchukuliwa eneo hilo lililokuwa eneo la Mbunge wa enzi hizo Edward Mwani ambaye alifidiwa eneo jingine na serikali. Kwa serikali ipo kwenye mpango wa kuboresha kilimo kupitia jeshi la magereza kwa kuliwezesha kuzalisha chakula cha kutosheleza kulisha wafungwa na mahabusu hivyo eneo la Matongo lipo kwenye orodha ya maeneo yaliyopewa kipaumbele katika kilimo cha mahindi, alizeti, pamba, ufugaji wa nyuki na mifugo pamoja na upandaji wa miti na uhifadhi wa mazingira, serikali ilichukua eneo hilo ili kuwezesha magereza kuendeleza shughuli za uelimishaji wa wafungwa kwa kutumia kilimo na ufugaji kwa sasa eneo hili limepimwa na taratibu za kupatikana kwa hati zinaendelea hivyo serikali haina mpango wa kurejesha eneo hilo kwa vijiji tajwa" alisisitiza Masauni
Majibu ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni yalimuinua tena Andrew Chenge na kutaka kufahamu ni lini serikali itakuwa tayari kuanza mpango huo kwani ni miaka mingi imeshindwa kufanya hivyo.
"Mhe. Spika gereza na Matongo ni gereza ambalo ni miongoni mwa magareza yaliyoanzishwa na serikali katikati ya miaka ya 70 kwa lengo hilo hilo ambalo waziri amelisema lakini zaidi ya miaka 40 ukifika pale Matongo hakuna cha maana kinachoendelea na Mhe. Waziri katika majibu yake anasema gereza hili lipo kwenye mpango wa kuboresha kilimo sasa ni lini mpango huu mahususi kwa gereza la Matongo utaanza kutekelezwa na serikali" alihoji Andrew Chenge