Kocha George Lwandamina ameshaitema klabu ya Yanga na tayari ZESCO United imeshatangaza rasmi kumsaini kocha huyo ambaye aliisaidia Yanga kushinda taji la ligi kuu Tanzania bara msimu wa 2016/17. Kinachoibua maswali mengi ni sababu za Lwandamina kuondoka kipindi hiki wakati Yanga ikiwa katika kipindi muhimu cha kutetea ubingwa wa ligi na kutafuta nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya kombe la shirikisho Afrika.
Ishu ya kwa nini Lwandamina ameondoka ndiyo gumzo kwa sasa, watu wengi wanataja kwamba kocha huyo ameondoka kutokana na hali mbaya ya uchumi ndani ya klabu hiyo na pengine hajalipwa mishahara na stahiki zaka mbalimbali ndiyo maana ameamua kusepa.
Shaffihdauda.co.tz imezinyaka taarifa za kuaminika kutoka ndani ya uongozi wa Yanga kwamba kuondoka kwa Lwandamina hakuhusiani kabisa na masuala ya maslahi yake binafsi, Katibu Mkuu wa klabu hiyo ndiyo anatajwa kuwa sababu kuu ya kutimka kwa Lwandamina.
“Katibu ndio chanzo cha kuondoka kwa Lwandamina, Mkwasa na Lwandamina hawakuwa sawa kwa muda mrefu sasa na wallikuwa hawazungumzi. Kifupi ni kwamba hawakuwa na ushirikiano kila mtu alikuwa anafanya mambo yake kivyake”-kimeeleza chanzo hicho na kuomba hifadhi ya jina lake.
“Ilifika wakati Lwandamina akatoa sharti kwamba kutokana na hali ilivyo Yanga wanatakiwa kuchagua jambo moja, aondoke yeye (Lwandamina) au aondoke Mkwasa. Naona ameamua kuondoka yeye kwa sababu ZESCO walikuwa wanamhitaji tangu siku nyingi nadhani baada ya kuona hakuna uwezekano Mkwasa akatoka Yanga ameamua kujiondoa yeye.”
Lwandamina ameondoka Yanga ikiwa zimebaki zimebaki mechi saba klabu hiyo imalize mechi za ligi lakini inakabiliwa na mchezo muhimu wa marudiano dhidi ya Wolaitta Dicha kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kombe la shirikisho Afrika. Mchezo wa awali uliochezwa Dar, Lwandamina alioongoza Yanga kushinda 2-0, mchezo wa marudiano utachezwa jijini Awasa Ethiopia Aprili 18, 2018 na kuamua timu gani itafuzu hatua ya makundi.