Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amewataka wanaume wote wanaochepuka na kunyanyasa familia zao waache mara moja kitendo hicho kwani sio kitendo cha kiungwana kwa mwanaume anayejitambua.
RC Gambo amewashauri wanaume wote wenye tabia hizo kuacha mara moja na kama watashindwa basi ni bora wakafanya mambo yao kimya kimya na kuheshimu familia zao kwani vitendo hivyo husababisha magonjwa kwenye familia.
“Familia nyingi zipo kwenye mateso kutokana na matendo ya wanaume. Nadhani haya mambo ni sababu kubwa za Presha na sukari kwa familia nyingi. Wanaume ni busara kuheshimu nyumba yako hata kama una vituko vyako.“ameeleza RC Gambo kwenye ukurasa wake wa Instagram na kusisitiza.
“Mwanamke mnaanza nae maisha, mnateseka nae mkiwa hamna chochote halafu Mungu anakupa riziki unaamua kumtesa mkeo. Wakati mwingine mwanaume unachukua hata chakula Cha ndani (unga , mchele, sukari na nk) alichokihangaikia mkeo kwa ajili ya watoto wake na kupeleka nyumba NDOGO.“ameandika Gambo.
Kwa upande mwingine Gambo amesema huu ni muda muafaka kuliangalia tatizo hilo kitaifa kwani familia nyingi zimekumbwa na janga hilo, “Kama Taifa tunahitaji tiba mbadala ya kuzisaidia familia zetu!“.