Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia baraza kuu la uongozi Mkoa wa Morogoro limemvua James Mkude nafasi aliyekuwa akiishika ya Mwenyekiti wa Wilaya ya Morogoro kutokana na tuhuma za kujihusisha na matukio yaliyo kinyume na katiba ya chama hicho.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Mlimba Bi. Suzani Kiwanga na kusema hatua hiyo imekuja baada ya kujiridhisha na tuhuma zilizo wasilishwa ndani ya chama hicho ingawa ni tuhuma binafsi zinazomkabili mwenyekiti huyo aliyesimamishwa na kwamba hazihusiani na chama.
Akitoa maadhimio ya wajumbe wa baraza la uongozi la chama hicho mkoa wa Morogoro waliokutana kujadili muenendo wa mwenyekiti huyo, Bi. Suzani amesema kuwa kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ya mwaka 2006 toleo la mwaka 2016 kifungu cha saba pamoja na maadili ya uongozi kinatoa mamlaka kwa baraza hilo kumsimamisha mtu yeyote atakae kiuka maadili ya kinidhamu ya chama hicho.