Lechantre, raia wa Ufaransa, ameiweka Yanga kiporo baada ya kusema kuwa, mechi hiyo itakuja kuamua bingwa wa ligi kuu msimu huu kama wote wawili watavuka salama mechi za hapa kati.
Simba na Yanga ambazo zinatarajiwa kupambana Aprili 29, mwaka huu, kwa sasa zote zina pointi 46 ambapo Simba inaongoza ikiwa na mabao mengi ya kufunga.
Kabla ya Aprili 29, Simba itacheza dhidi ya Njombe Mji, Mtibwa Sugar, Mbeya City, Prisons na Lipuli, huku Yanga ikicheza na Singida United, pamoja na mechi mbili za kimataifa za Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Wolaitta Dicha ya Ethiopia.
Lechantre amesema: “Mechi dhidi ya Yanga ipo mbali, hivyo kama wote tukivuka salama hapa kati ni wazi mechi hiyo itaamua nani bingwa msimu huu.”
Simba ambayo ili msimu ujao ishiriki michuano ya kimataifa kama msimu huu, inatakiwa iwe bingwa wa ligi kuu tofauti na wenzao Yanga ambao kwa sasa wana nafasi tatu za kuiwakilisha nchi kimataifa msimu ujao.
Nafasi ya kwanza ni kwenye Kombe la FA ambapo jana Jumapili walitarajiwa kucheza robo fainali dhidi ya Singida United, pia wana nafasi kwenye ligi kuu kama wakiwa mabingwa, lakini pia katika Kombe la Shirikisho ikitokea wamefika fainali na kuwa mabingwa wataiwakilisha tena nchi.