Kiongozi wa chama cha upinzani cha ODM Raila Odinga Ijumaa amekutana na kufanya mazungumzo na rais mstaafu Mwai Kibaki ambaye alishirikiana naye kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Ajenda ya kikao chao cha dharura, ambacho kimekuja mwezi mmoja tangu Odinga ashikane mkono na Rais Uhuru Kenyatta, haikuwekwa wazi.
Odinga aliongozana na Paul Mwangi mshauri wake wa masuala ya kisheria na mwenyekiti mwenza wa timu iliyoandaa mpango wa kiongozi huyo kushikana mkono na Kenyatta.
“Raila anakwenda kukutana na rais mstaafu,” Mwangi aliliambia kwa simu gazeti la Nation bila kutoa maelezo zaidi.
Hata hivyo, gazeti hilo, lilifahamishwa kwamba Odinga alitarajiwa kumfahamisha rais mstaafu juu ya mpango huo mpya na Kenyatta.
“Ni kuhusu suala la kushikana mkono, mambo mengine yanapita hivyo anataka kumweleza Mzee Kibaki kilichojiri,” kilisema chanzo kingine.
Kikao hicho pia kinafanyika wiki moja tangu Odinga awe na mazungumzo kama hayo na mrithi wa Mzee Kibaki, rais mstaafu Daniel Moi, nyumbani kwake Kabarak katika Kaunti ya Nakuru.
Mapema asuhubi leo Ijumaa, Odinga alikuwa na kikao na gavana wa Nairobi, Mike Sonko katika ofisi za Capitol Hill.