Benchi la ufundi la klabu ya Simba kesho litaingia kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Lupili FC likiwa na tahadhari kubwa kwa wachezaji wake wawili, mshambuliaji Emmanuel Okwi na kipa Aishi Manula kutoka na nyota hao kuwa na kadi mbili za njano.
Wawili hao tayari wameshaoneshwa kadi mbili za njano katika michezo miwili iliyopita na endapo wataoneshwa kadi nyingine ya njano katika mchezo wa kesho moja kwa moja watakuwa wamekosa mchezo ujao ambao ni dhidi ya Yanga April 29.
Benchi la ufundi la Simba huenda likachukua maamuzi magumu kuepusha nyota hao kupata kadi ambapo golini anaweza kuanza golikipa namba mbili Said Mohammed ambaye hajadaka mchezo hata mmoja msimu huu.
Kwa upande wa Okwi, makocha Pierre Lechantre na Masoud Djuma wanaweza kuamua kumwacha nje Okwi ambaye hana rekodi nzuri kwenye viwanja vya mikoani akiwa amefunga mabao matatu tu kati ya 19 ambayo amefunga msimu huu.
Simba kwasasa inaongoza ligi ikiwa na alama 58 kwenye michezo 24 ikifuatiwa na Yanga yenye alama 47 kwenye michezo 22. Lipuli FC ipo katika nafasi ya 8 ikiwa na alama 31 baada ya michezo 25.