Rais JPM Awajibu Wabunge Wanaobeza Serikali Kukopa

Rais JPM Awajibu Wabunge Wanaobeza Serikali Kukopa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Watanzania kutowasikiliza Wabunge wanaosema serikali inadaiwa madeni ilhali wao wanapita katika barabara hizo kuelekea bungeni.



Rais Magufuli amesema kuwa hata katika ukopaji unaweza ukakopa leo na ukalipa baada ya miaka 40 au 50 huku akieleza kuwa madeni anayokopa yeye huenda yakalipwa yeye hayupo duniani.

Rais Magufuli ameyasema hayo mjini Iringa alipofungua barabara ya Lami ya Iringa – Migoli- Fufu inayounganisha mikoa ya Iringa na Dodoma.

“Kwahiyo mimi nataka niwaeleze ukweli ndugu zangu, lile deni walilokopa wakoloni waingereza kwa kujenga ile barabara ya Morogoro Road kule Dar es salaam deni lake limemalizika mwaka juzi amelimaliza Kikwete, deni lilikopwa kwaajili ya uhuru kile kipande na si barabara yote kwahiyo unaweza ukakopa leo ukalipa baada ya miaka labda 40 hata miaka 50 madeni tunayolipa sasa hivi yanayolipwa yamekopwa katika awamu hizo zote,“ amesema Rais Magufuli.

“Inawezekana awamu ya madeni ninayo kopa yatalipwa wala mimi sipo duniani na ndio maana huwa mnawasikia wengine wanazungumza serikali inadaiwa madeni na huwa wanasahau wengine wanatoka huku Iringa wanaitumia hiyo hiyo barabara kwenda Bungeni, wanaitumia barabara hiyo hiyo kwa magari yao waliyoyapata waliyokopeshwa lakini wakiisha fika kule wanasema serikali inadaiwa madeni wanasahau kuwa hayo madeni ni pamoja na barabara waliyoipitia wakati wanaenda Bungeni.“
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad