Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefunguka na kusema kuwa makanisani saizi zaka zimepungua kwa kuwa mafisadi ndio walikuwa wanatoa zaka na kudai kuwa watu ambao walikuwa wamezoea kupata pesa za bure ndiyo wanapiga makelele.
Rais Magufuli amesema hayo jana alipokuwa akihutubia uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, wakati akiweka jiwe la msingi kwa ajili ya mradi wa kuongozea ndege katika vituo vinne hapa nchini.
"Ni uhakika pia wapo watu ambao walizoea fedha za bure za kuibia masikini wale ndio wanapiga kelele kweli.
"Nina fahamu hata makanisani zaka zimepungua kwa sababu zingine zilikuwa zinatolewa na mafisadi, lakini sisi Watanzania tusimame twende mbele .Ninawaeleza kwa dhati kwa sababu najua tulikotoka na tunakokwenda. Watendaji wangu hawa wanafanyakazi kubwa kweli" alisema Rais Magufuli
Mbali na hilo Rais Magufuli alisema kuwa nchi sasa ipo salama kutokana na jitihada za maafisa wa ulinzi na usalama na kusema anashangaa kuona watu wakati wa mauaji wa kibiti hawatoi waraka.
"Wakati wa mauaji ya Kibiti hatukuona mtu yoyote analaani, kufa kwa Kibiti ni salama hakuna hata waraka uliotoka ingawaje sipendi sana kulizungumzia hili kwa sababu nalijua wala halina msingi sana na wala halitafanikiwa na wala hakuna lolote kwa sababu serikali ipo na nimekabidhiwa na wananchi kuilinda kwa nguvu zote na ninasema kweli kweli wengine nawaangalia tu"