Rais
John Magufuli jana alimmwagia sifa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda
kwa kumwelezea ni kiongozi mkimya na asiyependa kuzungumza ovyo ovyo.
Rais
Magufuli alisema Pinda, maarufu kama Mtoto wa Mkulima, ni kiongozi
anayefaa kuigwa na viongozi wengine, na kwamba hata yeye siku akistaafu
atamfuata ili kujifunza.
Aliyasema
hayo jana mjini Dodoma wakati akifungua Tawi la Benki ya NMB la
Kambarage na Jengo la Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF).
“Mzee
Pinda anaishi maisha ya kawaida sana, hapigi kelele, hazungumzi
chochote, Mzee Pinda ‘you are too special’ (wewe ni mtu wa kipeke),”
alisema Rais Magufuli.
“Watu
watakukumbuka (Pinda) kwa ukarimu wako, wewe ni mtu wa kawaida sana.
Sasa hivi hatujui thamani yako lakini ipo siku tutaijua.
“Ndiyo
maana bado unaonekana kijana, hujipi ‘pressure’ (hofu), unaamini kile
unachofanya, na mimi nikistaafu nitakuja kuchukua ‘course’ (mafunzo)
kwako.”
Sifa
kwa Pinda zinakuja miezi saba tangu alipokosoa viongozi wastaafu wa
"maeneo mengine" wanaosemasema kila wakati kuhusu uendeshaji wa
serikali.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam Septemba 11, mwaka jana Rais Magufuli alitoa mfano
wa majaji wastaafu ambao alisema ni tofauti na wastaafu wengine na
kwamba huenda kujua sheria ndiko kunakowasaidia kutokuwa waropokaji.
Rais Magufuli alisema hayo wakati wa kumuapisha Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma.
“Nawashuruku
majaji wakuu wastaafu, Barnabas Samatta na Augustino Ramadhani,
walifanya kazi kubwa ya kujenga misingi ya mahakama nchini," alisema.
“Bahati
nzuri majaji hawa ni waadilifu sana huwezi kumsikia Jaji (Mkuu mstaafu
Othman) Chande, (Barnabas) Samatta, Augustino (Ramadhani), (Damian)
Lubuva au majaji walioko hapa... ukiangalia wastaafu wa maeneo mengine
hawachoki kusema, wanawashwawashwa.
“Ndiyo
maana nawapongeza sana mahakama...Ni safi mno, nina uhakika wanapotaka
kutoa ‘advice’ (ushauri) yoyote (wowote) lazima wanakushirikisha (Jaji
Mkuu); ndiyo faida ya kujua sheria.
“Sisi wengine huku ambao hatujajua sheria mahali popote, chochote unaweza ukazungumza.”