Rais wa Korea Kaskazini Avuka Mpaka na Kuingia Korea Kusini

Kim Jong-un amekuwa kiongozi wa kwanza wa Korea Kaskazini kuingia Korea Kusini kwa kuvuka mstari wa kijeshi uliowekwa kugawanya mataifa hayo mawili tangu vita vya Korea 1953.

Katika hatua ilioshangiliwa kwa mbwembwe za kila aina kiongozi wa Korea Kusini na mwenzake wa Korea Kaskazini walisalimiana kwa mikono katika mpaka huo.

Bwana Kim alisema kuwa anatumai kwamba kutakuwa na mazungumzo ya kufana baada ya ufunguzi mzuri wakati mazungumzo hayo yalipoanza.

Mkutano huo wa kihistoria utaangazia maswala ya silaha za kinyuklia na uwezekano wa makubaliano ya amani.

Mengi yatakayozungumzwa ni mambo ambayo tayari yameafikiwa awali lakini wachanganuzi wengi bado wana wasiwasi kuhusu uaminifu wa Korea Kaskazini katika kukubalia kuacha shughuli ya utengezaji wa silaha za kinyuklia.

Hatahivyo shughuli zote za taifa lote la Korea Kusini zilisimama kwa muda ambapo viongozi hao wawili walisalimiana kwa mikono katikati ya mpaka wa mataifa hayo mawili.

Na baadaye watu walishangaa baada ya bwana Kim kumualika kiongozi wa Korea Kaskazini kuvuka kwa muda mfupi katika mstari wa mpaka wa mataifa hayo mawili kuingia Korea Kaskazini, kabla ya wawili hao kurudi tena Korea Kusini muda wote huo wakiwa wameshikana mikono.

NI mara ya kwanza kwa viongozi wa Korea kukutana kwa zaidi ya muongo mmoja.
'Mwanzo wa historia mpya'

Viongozi hao wawili walikutana na gwaride ambalo likikuwa limevalia nguo za kitamaduni upande wa taifa la Korea Kusini.

Wawili hao baadaye walielekea katika jumba la amani huko Panmunjom, eneo la kijeshi katika mpaka huo ili kuanza mazungumzo.

Historia mpya imeanza sasa katika mwanzo wa amani, ulisema ujumbe ulioandikwa na bwana Kim alioandika katika kitabu cha wageni ndani ya jumba hilo la amani.

Uzito wa mkutano huo ukiwa ni wa kwanza kati ya viongozi hao wa Korea katika zaidi ya muongo mmoja pia haukukosa ucheshi.

Bwaana Kim alifanya mzaha kuhusu kuleta tambi za baridi katika mkutano huo.

''Nadhani utapendelea sana tambi tulizoleta'', alisema. Ikulu ya Whitehouse imesema kuwa inatumai kwamba mazungumzo hayo yatapiga hatua.

Mkutano huo wa Korea unaonekana kuwa maandalizi ya mkutano kati ya Kim Jong Un na rais wa Marekani Donald Trump, mapema mwezi Juni, hatua isiokuwa ya kawaida kwani hakuna rais wa Marekani ambaye aliwahi kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini.

Top Post Ad

Below Post Ad