Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un anakuwa Kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo kuingia nchini Korea Kusini tangu kumalizika vita vya Korea, mwaka 1953.
Korea Kusini imesema Rais Moon Jae-in atakutana ana kwa ana na rais Kim kwenye mpaka kati ya nchi hizo mbili, siku ya Ijumaa.
Mzungumzo hayo ya kihistoria yatalenga nia ya hivi karibuni ya Korea Kaskazini ya kuachana na silaha za nuklia.
''Ugumu uko kwenye kufahamu ni kwa kiasi gani watafikia makubaliano kuhusu utayari wa kuachana na silaha za nuklia'' alieleza msemaji wa rais wa Korea Kusini, Im Jong-seok.
Watu walishangaa kumuona Dada yake Rais Kim, Kim Yo-jong mjini pyeongchang
Mkutano huo wa tatu baada ya mkutano wa mwaka 2000 na 2007 ni matokeo ya jitihada zilizofanyika miezi kadhaa kuimarisha mahusiano kati ya Korea hizi mbili na kufungua milango ya mkutano kati ya Kim na Rais wa Marekani Donald Trump.
Kim alitangaza juma lililopita kuwa angesitisha zoezi la majaribio ya silaha za nuklia kwa sasa.Hatua hiyo ilikaribishwa na Marekani na Korea Kusini kama hatua nzuri,ingawa watafiti wa China wameonyesha kuwa eneo linakofanyika jaribio la nuklia la Korea Kaskazini huenda lisitumike tena baada ya mwamba kuporomoka baada ya jaribio la mwisho la mwezi Septemba.
Viongozi hao pia wanatarajiwa kujadili njia za kupata amani katika eneo la Peninsula na kuhitimisha rasmi vita vya Korea vya mwaka 1950-1953, na maswala ya uchumi na kijamii.
Korea Kusini na Marekani zimesema zinasitisha mazoezi ya kijeshi kwa siku moja kupisha mkutano huo.
Kim ataongozana na maafisa tisa, akiwemo dada yake, Kim Yo-jong,aliyeongoza ujumbe wa Korea Kaskazini kwenye michuano ya Olimpiki nchini Korea Kusini mapema mwaka huu.Mkutano huu pia utawahusisha maafisa wa juu wa kijeshi na wanadiplomasia.
''Naona Korea Kaskazini inawapeleka maafisa wa kijeshi pia, Korea inaamini kuwa kusitishwa kwa mpango wa nuklia ni jambo muhimu''.alieleza msemaji wa Korea kusini.
Korea Kusini itapeleka maafisa saba wakiwemo mawaziri wa ulinzi,mambo ya nje na muungano.Mkuu wa majeshi ni sehemu ya ujumbe huo.
Rais wa Korea Kaskazini Kukutana na Mwenzake wa Kusini
April 26, 2018
Tags